Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM – Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimeendelea kujiimarisha katika sekta ya uchukuzi baada ya kuanzisha rasmi mafunzo ya urubani nchini, hatua iliyotajwa kuwa suluhisho la changamoto ya gharama kubwa za masomo ya fani hiyo nje ya nchi.
Hatua hiyo imepongezwa na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa (Mb), alipohutubia Mahafali ya 41 ya chuo hicho, yaliyoshuhudia zaidi ya wahitimu 4,000 wakivikwa taji katika ngazi mbalimbali za elimu.
Alisema Serikali tayari imekabidhi ndege tatu kwa ajili ya mafunzo, sambamba na kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya usafiri wa anga, reli, barabara, maji na mabomba ili kuendana na kasi ya maendeleo ya sekta hiyo.
Waziri huyo alieleza kuwa NIT imepanua mafunzo yake katika nyanja tano kuu za usafirishaji, akisisitiza kuwa chuo hicho kinabeba jukumu kubwa la kuzalisha wataalamu watakaosimamia miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali.
Katika hotuba yake, Prof. Mbarawa aliwataka wahitimu kutumia maarifa waliyoyapata kwa uadilifu na uzalendo, huku wakilinda amani na mshikamano wa taifa kama msingi wa maendeleo endelevu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji, Dkt. Prosper Mgaya, alisema ongezeko la udahili kwa zaidi ya asilimia 35 katika kipindi cha miaka mitano ni matokeo ya mageuzi yanayoendelea kufanywa chuoni hapo ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira.
Aliongeza kuwa kupitia ufadhili wa Serikali na washirika wa maendeleo, chuo kimefanikiwa kujenga miundombinu ya kisasa ikiwemo Kituo cha Umahiri cha Usafiri wa Anga na Operesheni za Usafirishaji, mabweni, maabara na karakana.
Dkt. Mgaya alisema NIT pia inaendelea kusogeza huduma zake karibu na wananchi kupitia ujenzi wa kampasi mpya katika mikoa ya Kilimanjaro na Lindi, lengo likiwa ni kuongeza idadi ya wataalamu wa sekta ya uchukuzi katika ngazi mbalimbali.
Mahafali ya 41 ya NIT yamefanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 50 ya chuo hicho, ambayo yameacha alama ya mchango wake mkubwa katika kukuza sekta ya uchukuzi na usafirishaji nchini.







