Featured Kitaifa

WAKAGUZI WA NDANI WAPONGEZWA KWA KUSIMAMIA VYEMA MIRADI YA MAENDELEO

Written by Alex Sonna

Mkaguzi wa Mkuu wa Ndani wa Serikali Msaidizi, Mhandisi Kenneth Nindie, akizungumza jambo wakati akifunga mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo Wakuu wa Vitengo vya Ukaguzi na Wakaguzi Wakuu wa Ndani kutoka Wizara, Sekretarieti za Mikoa, Halmashauri na Taasisi mbalimbali za Serikali zaidi ya 90, yaliyofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Cate, mjini Morogoro.

Mwenyekiti wa Mafunzo ya Wakaguzi wa Ndani wa Serikali, Bw. Jackson Kingumwile, akitoa neno la shukrani wakati wa kufunga mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo Wakuu wa Vitengo vya Ukaguzi na Wakaguzi Wakuu wa Ndani kutoka Wizara, Sekretarieti za Mikoa, Halmashauri na Taasisi mbalimbali za Serikali zaidi ya 90, yaliyofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Cate, mjini Morogoro.

Baadhi ya Wakuu wa Vitengo vya Ukaguzi na Wakaguzi Wakuu wa Ndani kutoka Wizara, Sekretarieti za Mikoa, Halmashauri na Taasisi mbalimbali za Serikali zaidi ya 90, wakifuatilia hotuba ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali Msaidizi, Mhandisi Kenneth Nindie (hayupo pichani) wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo Wakuu wa Vitengo vya Ukaguzi na Wakaguzi Wakuu wa Ndani wa Serikali, katika ukumbi wa hoteli ya Cate, mjini Morogoro.



Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali Msaidizi, Mhandisi Kenneth Nindie (Katikati aliyeketi), akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Vitengo vya Ukaguzi na Wakaguzi Wakuu wa Ndani kutoka Wizara, Sekretarieti za Mikoa, Halmashauri na Taasisi mbalimbali za Serikali zaidi ya 90, baada ya kufunga mafunzo ya kuwajengea uwezo Wakuu wa Vitengo vya Ukaguzi na Wakaguzi Wakuu wa Ndani wa Serikali, katika ukumbi wa hoteli ya Cate, mjini Morogoro.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Morogoro)

Na. Joseph Mahumi, Morogoro

Wakaguzi wa ndani wa Serikali wamepongezwa kwa kusimamia vyema miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali kwa kuhakikisha miradi hiyo inakua na ubora unaolingana na thamani halisi ya fedha.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali Msaidizi, Mhandisi Kenneth Nindie wakati akifunga mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo Wakuu wa Vitengo vya Ukaguzi na Wakaguzi Wakuu wa Ndani kutoka Wizara, Sekretarieti za Mikoa, Halmashauri na Taasisi mbalimbali za Serikali, yaliyofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Cate, mjini Morogoro.

Mhandisi Nindie alisema kuwa wakaguzi wa ndani wamekuwa imara na wazalendo kwa kuwa wanahakikisha miradi ya maendeleo inakua na matokeo mazuri kwa kuhakikisha kila hatua ya ukaguzi ina matokeo chanya yanayoakisi thamani ya mradi.

“Niwatake sasa kupitia mafunzo haya ya siku tatu mliyoyapata muendelee kuongeza ufanisi zaidi katika kukagua miradi ya taasisi zenu ili tuweze kupata matokeo mazuri katika miradi ya maendeleo lakini pia kuwatumikia wananchi wetu wapate miradi bora kwa maslahi mapana ya Taifa” alisema Mhandisi. Nindie.

Aidha, alilisitiza kuwa wakaguzi waendelee kuwa wazalendo na kulitumikia Taifa katika nafasi yao ili kuhakikisha Tanzania inafikia malengo yake ya muda mrefu na muda mfupi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mafunzo hayo, Bw. Jackson Kingumwile, alisema kuwa Mafunzo hayo yamewajengea uwezo mkubwa na wanaona dhana za Ukaguzi wa Mazingira, Kijamii na Utawala Bora (Environmental, Social, and Governance-ESG) pamoja na Ukaguzi wa Thamani ya Fedha (Value for Money-VFM), si nadharia tu, bali ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha miradi na programu za serikali inaleta matokeo chanya kwa jamii, inalinda mazingira, na inaendeshwa kwa misingi imara ya utawala bora.

“Tumepata uelewa wa kina juu ya namna ya kutambua hatari za kimazingira na kijamii, umuhimu wa uthabiti pamoja na wajibu wetu wa kuhakikisha thamani halisi ya fedha inapatikana katika kila hatua ya utekelezaji wa miradi” alisema Bw. Kingumwile.

Aliongeza kuwa, Wizara ya Fedha kupitia Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, iendelee kuandaa mafunzo kama hayo kwa kuwa wakufunzi walikua mahiri, wenye weledi, uzoefu na namna nzuri ya kuwasilisha mada kwa uhalisia unaoendana na mazingira ya utendaji wa Taasisi za Umma.

About the author

Alex Sonna