Featured Kitaifa

RAIS SAMIA: JENISTA MHAGAMA ALITANGULIZA MASLAHI YA TAIFA MBELE

Written by Alex Sonna

Na.Alex Sonna-DODOMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema marehemu Jenista Mhagama, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Peramiho, alikuwa kiongozi wa mfano aliyekuwa akitanguliza maslahi ya Taifa mbele ya maslahi binafsi, akieleza kuwa mchango wake umeacha alama kubwa katika uimarishaji wa Taifa na utendaji wa Serikali.

Akizungumza leo wakati wa shughuli ya kuuaga mwili wa marehemu Mhagama, Rais Samia amesema Taifa limepoteza kiongozi mahiri, jasiri na mwenye nidhamu, aliyelitumikia Bunge na Serikali kwa moyo wa uzalendo na uwajibikaji wa hali ya juu.

Rais Samia amesema marehemu alipendwa na kuheshimiwa na watu wote, hususan wale waliokuwa chini ya uongozi wake, kutokana na utendaji wake uliotukuka na uwezo wake wa kutatua changamoto kwa ufanisi. Amesema alimpa jina la “kiraka” kwa sababu kila alipowekwa alitimiza majukumu yake kwa usahihi na matokeo chanya.

“Mhe. Jenista Mhagama alikuwa akitanguliza maslahi ya Taifa kabla ya kitu kingine chochote. Sehemu ya uimara wa Taifa tulionao leo umechangiwa na uchapakazi wake mkubwa,” amesema Rais Samia.

Ameongeza kuwa mafanikio ya Bunge na Taifa kwa ujumla hutokana na mshikamano wa viongozi wote, wakiwemo wabunge na mawaziri, bila kujali tofauti za kisiasa au mitazamo binafsi. Amesema marehemu alifanya kazi kubwa kwa nchi na alikuwa mlezi wa wengi ndani ya Bunge na Serikali kwa ujumla.

Rais Samia pia amemtaja marehemu Jenista Mhagama kuwa nguzo ya matumaini kwa wanawake na vijana, akisisitiza kuwa alikuwa kiongozi aliyekuwa anahimiza nidhamu, uwajibikaji na kujituma katika utendaji wa umma.

Aidha, Rais ametoa pole kwa familia ya marehemu, wananchi wa Peramiho, wabunge na Watanzania wote kwa msiba huo, akiahidi kuwa Serikali itaendelea kuthamini na kulinda mchango wa viongozi waliolitumikia Taifa kwa uaminifu na kujitoa kama alivyofanya marehemu Mhagama.

Hafla ya kuuaga mwili imefanyika kwa heshima kubwa, ikihudhuriwa na viongozi wa kitaifa, wabunge, viongozi wa dini, ndugu, jamaa na wananchi, kabla ya mazishi kufanyika baadaye.

About the author

Alex Sonna