Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI na Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Disemba 11, 2025 wamekutana jijini Dodoma kujadili kwa pamoja mikakati ya kuimarisha ushirikiano katika kuwawezesha vijana wa Tanzania kupata fursa za elimu, ujuzi na ajira.
Kikao hicho kimeongozwa na Prof. Carolyne Nombo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, pamoja na Jenifa Omolo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana.
Viongozi hao wamejadili njia za kuhakikisha vijana wanapata taarifa sahihi kuhusu fursa za elimu na kuwezeshwa ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Prof. Nombo amesema kuwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 Toleo la 2023 pamoja na mitaala iliyoboreshwa vinaendelea kumwandaa kijana wa Kitanzania kupata ujuzi unaohitajika katika ulimwengu wa kazi.
Amesisitiza kuwa sera hiyo inatoa nafasi kwa vijana wote, wakiwemo walioacha shule awali, kurejea na kupata elimu kupitia mfumo rasmi na usio rasmi, ikiwemo programu ya IPOSA.
Aidha, Prof. Nombo amebainisha kuwa Serikali inaendelea kupanua fursa za ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, mikopo ya elimu, pamoja na ufadhili kupitia Samia Skolashipu, ili kuongeza wigo wa vijana kupata elimu na ujuzi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Jenifa Omolo, ameipongeza Wizara ya Elimu kwa kuanzisha programu nyingi zinazolenga kuwawezesha vijana kujitegemea na kushindana katika soko la ajira. Amesema programu hizo ni muhimu katika kuchochea ushiriki wa vijana katika uchumi wa taifa.
Katika kikao hicho, viongozi hao wamekubaliana kuimarisha upatikanaji wa taarifa za fursa mbalimbali kwa vijana, kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya kugharamia mafunzo mahususi, pamoja na kuratibu programu zitakazowaunganisha vijana na viwanda ili kupata mafunzo kwa vitendo.
