Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Saba Dk. Ali Mohamed Shein amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni alipomtembelea nyumbani kwake Zanzibar, Disemba 10,2025 ambaye aliambatana na viongozi mbalimbali kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.
Mwandishi Wetu,Zanzibar
Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi awamu ya sita Dk. Amani Abeid Karume pamoja na Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Awamu ya Saba Dk. Ali Mohamed Shein wameitaka Ofisi ya Makamu wa Rais kuendelea kutoa elimu ya kutosha ya Muungano ili misingi ya Muungano iliyowekwa na waasisi iendelee kudumishwa.
Marais wastaafu hao, Wameyasema hayo kwa nyakati mbili tofauti Disemba 10, 2025 wakati Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni alipowatembelea viongozi hao huku akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa Ofisi ya Makamu wa Rais.
Mhe. Dk. Karume amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuuendeleza umoja huu hususani katika ulimwengu wa sasa, hii itasaidia kuwa na umoja zaidi na hili ndio litatufanya kuwa imara kwa kuangalia mifano ya mataifa mengine.
Mhe. Karume amesema wengi wanauonea wivu Muungano wetu hivyo kitakachotusaidia ni kuendelea kuimarisha umoja, mshikamano na kuendelea kuwaelimisha vijana wetu ili wafahamu sababu na umuhimu wa kuwepo kwa Muungano.
“Sisi tuliokuwepo tulibahatika kuwauliza wazee wetu sababu ya wao kuuweka Muungano huu, lakini vijana hawa wanapaswa nao wafahamishwe faida na misingi ya Muungano maana hawajui hivyo wanatakiwa kuelimishwa, hata sisi tulipofanikiwa kuingia kwenye uongozi tulihakikisha tunauimarisha umoja huo,”
Kwa upande wake Mhe. Dkt Shein amesema tumekuwa tukisahau na hatukumbushani nini kilichokuwa chanzo cha Muungano, hivyo ni vyema Ofisi ya Makamu wa Rais ikafanya jitihada ya kusaidia wengine kujua faida ya umoja huu na hii itasaidia kuudumisha Muungano wetu.
“Elimu ikitolewa vizuri itasaidia vijana ambao bado hawana uelewa wa kutosha wa Muungano wetu, kuelewa. Watu wengi ambao wamezaliwa baada ta Mwaka 1964 hawaufahamu Muungano na hiyo imepelekea wao kutoa kauli mbalimbali ambazo sio nzuri.
“Sababu kuwa ni kwamba hawajui misingi ya Muungano iliyowekwa na waasisi wetu, hivyo Ofisi ya Makamu wa Rais inalojukumu kubwa la kutoa elimu kwao.
Ikumbukwe Aprili 22, 1964 ndio siku ambayo hati ya Muungano ilisainiwa katika Ikulu ya Zanzibar na aliyekuwa Rais wa Tanganyika Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amman Karume.
Aprili 26, 1964, Jamhuri ya Tanganyika chini ya uongozi wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar chini ya uongozi wa Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, ziliafikiana kwa mkataba kuunganisha nchi hizi mbili huru kuwa nchi moja inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aprili 25, 1964 ndio siku ambayo hati ililidhiwa ambapo kwa Zanzibar ililidhiwa na Baraza la Mapinduzi na Bara iliridhiwa na Bunge la Tanganyika na kusainiwa na Mwl Nyerere Aprili 26, 1964. Hivyo ndio maana hadi leo Aprili 26 Taifa huadhimisha miaka kadhaa ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Saba Dk. Ali Mohamed Shein amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni alipomtembelea nyumbani kwake Zanzibar, Disemba 10,2025 ambaye aliambatana na viongozi mbalimbali kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.

Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Saba Dk. Ali Mohamed Shein (katikati) akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mazungumzo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (kushoto) alipomtembelea nyumbani kwake Zanzibar, Disemba 10,2025 ambaye aliambatana na viongozi mbalimbali kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.
PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS