Uncategorized

DKT.ABBASI ATAJA SIRI YA TANZANIA KUTWAA TUZO NYINGI ZA UTALII KIMATAIFA

Written by Alex Sonna

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, amesema uwekezaji uliofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uhifadhi na utalii umeiwezesha Tanzania kushinda tuzo mbalimbali za utalii duniani.

Ameyasema hayo leo Desemba 10,2025 katika kipindi cha Clouds 360 kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Clouds alipofanyiwa mahojiano maalum kwa njia ya simu.

“Rais Samia ameendeleza sekta ya utalii ikiwa ni pamoja na kushiriki katika filamu za Tanzania The Royal Tour, Amazingi Tanzania na pia kufanya uwekezaji katika maeneo mbalimbali ya hifadhi nchini,” Dkt. Abbasi amesisitiza.

Amefafanua kuwa Tanzania imeshinda tuzo kadhaa za Shirika la Utalii Duniani (World Travel Awards (WTA 2025), nchini Bahrain Desemba 6, 2025 ikiwa ni pamoja na kushinda kwa mara ya tatu mfululizo kama Nchi Inayoongoza Duniani kwa Utalii wa Safari.

Ametaja tuzo zingine ni Kisiwa mashuhuri cha Zanzibar (Spice Islands) kushinda Tuzo ya World MICE Awards 2025 kama Eneo Bora Afrika kwa Mikutano na Matukio ya Kitaasisi na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kutangazwa kuwa Hifadhi Bora ya Taifa Duniani 2025.

Ameongeza kuwa Tanzania imepata tuzo mbili zaidi katika kundi la Sekta Binafsi, ikiwemo Kampuni Bora ya Safari za Puto Duniani, iliyotwaliwa na kampuni ya Serengeti Balloon Safaris na Kisiwa bora cha Mapumziko Duniani na Jumaira Thanda Resort katika Kisiwa cha Mafia nchini Tanzania.

Kadhalika, Dkt. Abbasi ameweka bayana kuwa Tanzania ni miongoni mwa mataifa Barani Afrika yaliyoongeza watalii wengi kabla na baada ya Uviko-19.

About the author

Alex Sonna