Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya, Bw. Hamad Kaaya,akizungumza wakati akifungua mdahalo kuhusu changamoto za kimaadili kwa wanafunzi na ufumbuzi wake uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Mheshimiwa Almishi Hazali,

Katibu Msaidizi kanda ya kaskazini Arusha Bw. Gerald Mwaitebele ,akizungumza wakati wa mdahalo kuhusu changamoto za kimaadili kwa wanafunzi na ufumbuzi wake uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang

Baadhi ya washiriki wa kongamano wakisikiliza hotuba ya Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya, Bw. Hamad Kaaya (hayupo pichani) wakati akifungua mdahalo kuhusu changamoto za kimaadili kwa wanafunzi na ufumbuzi wake kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Mheshimiwa Almishi Hazali,

Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya, Bw. Hamad Kaaya,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua mdahalo kuhusu changamoto za kimaadili kwa wanafunzi na ufumbuzi wake kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Mheshimiwa Almishi Hazali,
…..
Wazazi, walezi na walimu nchini wametakiwa kukemea vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kwa kuhakikisha wanawapatia chakula, malezi bora, muda wa kuzungumza nao, kuwaelekeza, na kusimamia matumizi ya simu na mitandao ya kijamii.
Pia wametakiwa kushiriki kikamilifu katika mikutano ya shule, vikao vya wazazi na programu mbalimbali za malezi nchini.
Wito huo umetolewa na Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya, Bw. Hamad Kaaya, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Mheshimiwa Almishi Hazali, wakati akifungua mdahalo kuhusu changamoto za kimaadili kwa wanafunzi na ufumbuzi wake. Mdahalo huo umefanyika Desemba 5, 2025, katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang.
Akizungumza katika mdahalo huo, Bw. Kaaya ametaja baadhi ya changamoto zinazowakumba watoto kuwa ni pamoja na vitendo vya ukatili ikiwemo ubakaji, ambapo baadhi ya wazazi huamua kumaliza kesi hizo nje ya mfumo wa sheria. Changamoto nyingine ni kutopata chakula cha mchana mashuleni, migogoro ya kifamilia, ulevi, na wazazi kutengana.
Aidha, ameongeza kuwa matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yamekuwa chanzo cha watoto kupotoshwa na maudhui yasiyofaa kama ngono, ukatili, utapeli na lugha zisizostahili. Vilevile, ushawishi hasi wa makundi rika husababisha baadhi ya watoto kujiingiza katika utoro, uvutaji wa sigara, ulevi na vitendo vya ukosefu wa maadili.
“Hatua za msingi za kukabiliana na changamoto hizo kuwa ni pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kuripoti matukio ya ukatili na kuyafikisha kwenye vyombo vya sheria, kuzuia wazazi kumaliza kesi nje ya mfumo, kuimarisha ulinzi wa watoto mashuleni na katika jamii, kuzuia matumizi mabaya ya mitandao, pamoja na kutoa elimu ya malezi bora.”amebainisha Bw. Kaaya
Kwa upande wake, Katibu Msaidizi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kaskazini—Arusha, Bw. Gerald Mwaitebele, amewataka wazazi, walezi na walimu kuhakikisha watoto wanasimamiwa kikamilifu ili kukabiliana na ukatili unaofanywa na watu wasiokuwa waadilifu.
Mmoja wa washiriki wa mdahalo huo, ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Kateshi A, alitoa ushauri wa kuanzishwa kampeni maalumu zitakazohusu wajibu wa wazazi na madhara ya mmomonyoko wa maadili, hususan katika matumizi ya simu na mitandao ya kijamii kwa watoto wa shule.
Kongamano hilo limefanyika kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Duniani, yanayofanyika kila Desemba 10 kila mwaka.