Kitaifa

KAMBI YA UPASUAJI WA MASIKIO,PUA NA KOO YAZINDULIWA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA

Written by Alex Sonna

DODOMA

DODOMA,

KAMABI  ya matibabu ya upasuaji wa Masikio, Pua na Koo (ENT) inayoendeshwa kwa ushirikiano kati ya Madaktari Bingwa wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) na wenzao kutoka Shirika la Hands Giving Lives la nchini Uturuki imezinduliwa rasmi jijini Dodoma.

Akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kuzindua kambi hiyo, iliyonza Desemba 1 na kutarajiwa kuendelea hadi Desemba 7, 2025, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa wizara hiyo, Bw. Issa Ng’imba, amepongeza ushirikiano kati ya BMH na Shirika la Hands Giving Lives la Türkiye uliowezesha kufanyika kwa kambi hiyo ya ubingwa wa upasuaji wa masikio.

“Kambi hii imetoa fursa kwa wananchi kupata huduma za ubingwa bobezi wa upasuaji wa masikio, ambapo jumla ya wagonjwa 10 watafanyiwa upasuaji. Aidha, imewajengea uwezo madaktari bingwa wa BMH, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na madaktari kutoka hospitali za rufaa za mikoa ya Dodoma, Tabora na Manyara kupitia mafunzo maalumu yaliyotolewa na bingwa wabobezi kutoka Türkiye,” amesema  Bw. Ng’imba.

Aidha ametoa wito wa kupanua wigo wa ushirikiano huo ili kuhusisha maeneo mengine ya matibabu yenye uhitaji mkubwa, pamoja na kuongeza mikoa inayonufaika na mafunzo ya kujengewa uwezo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof. Abel Makubi, amesema kuwa upasuaji wa masikio (Temporal Bone Surgeries) utakaofanywa katika kambi hiyo ni miongoni mwa operesheni ngumu ambazo awali zilifanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili pekee, na kwa idadi ndogo ya wataalamu.

“BMH sasa inakuwa hospitali ya pili nchini kutoa huduma hii inayohitaji utaalamu wa hali ya juu, vifaa vya kisasa na umakini mkubwa. Wananchi wenye changamoto za kusikia na matatizo ya masikio watambue kuwa matibabu ya ubingwa wa juu sasa yanapatikana hapa nchini,” amesisitiza Prof. Makubi.

Aidha, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha mashirikiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Türkiye, pamoja na Wizara ya Afya, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na ubalozi wa Tanzania nchini Türkiye kwa kuratibu ushirikiano huo wenye tija.

Naye Rais wa Shirika la Hands Giving Lives na kiongozi wa timu ya madaktari bingwa kutoka Türkiye, Bi. Hatice Ozdemir, alisema nchi yake ina dhamira ya kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika maeneo mbalimbali ya huduma za afya. Aliongeza kuwa shirika lake liko tayari kupanua wigo wa ushirikiano na BMH zaidi ya upasuaji wa masikio, ikizingatiwa kuwa huduma hizo zinahitaji miundombinu na vifaa vya kisasa kama ilivyo katika BMH.

About the author

Alex Sonna