Featured Kitaifa

TUME YA USHINDANI YAPIGIA CHAPUO SHERIA NA SERA KATIKA ENEO LA AI

Written by Alex Sonna

Tume ya Ushindani (FCC) imezindua Wiki ya Ushindani ikiwa ni maandalizi ya Siku ya Ushindani Duniani itakayofanyika Desemba 5, huku ikilenga kutoa elimu kuhusu nafasi ya Akili Mnemba (AI) katika kudhibiti au kuchochea ushindani wa masoko.

Lengo kuu la maadhimisho hayo ni kuongeza uelewa wa umma na kuimarisha utekelezaji wa sera na sheria zinazolinda ushindani wenye manufaa kwa uchumi.

Akiongea jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, alisema maadhimisho haya yana asili yake katika uamuzi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la mwaka 1980 kupitia Kanuni za Kimataifa za Kukinga Vitendo vinavyokandamiza Ushindani, maarufu kama UN Set.

Amesema kanuni hizo zimekuwa msingi wa mifumo ya ushindani duniani na zimeisaidia Tanzania kujenga mazingira bora ya biashara.

Ngasongwa alieleza kuwa kupitia Sheria ya Ushindani Na. 8 ya mwaka 2003, FCC inaendelea kusimamia masoko ili kuhakikisha hakuna vitendo vinavyoweza kupunguza ushindani au kudhulumu watumiaji.

Kwa mujibu wa FCC, udhibiti huo unajumuisha kuchunguza makubaliano ya kibiashara, kuzuia matumizi mabaya ya nguvu ya soko na kuchambua miunganiko ya kampuni.

Sheria inazitaka kampuni zinazotaka kufanya muamala wa thamani ya Shilingi bilioni 3.5 au zaidi kuwasilisha taarifa kwa FCC kwa ajili ya tathmini ya ushindani, hatua inayolenga kuzuia ukiritimba na kulinda maslahi ya walaji.

Kwa mwaka huu, kaulimbiu iliyoteuliwa ni “Artificial Intelligence (AI), Consumers and Competition Policy)” ikilenga kuonesha athari za AI katika masoko na umuhimu wa kulinda haki za watumiaji.

       Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa

 

 

 

 

 

 

 

 

PICHA ZOTE NA JAMES SALVATORY – TORCH MEDIA 

About the author

Alex Sonna