WAZIRI wa Madini Mhe.Anthony Mavunde,akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 25,2025 jijini Dodoma kuhusu kufutwa kwa leseni kwa wachimbaji Madini nchini.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WAZIRI wa Madini, Mhe.Anthony Mavunde, ametangaza kufutwa kwa jumla ya leseni 73 za madini baada ya wamiliki wake kushindwa kurekebisha makosa na kutotekeleza wajibu wao kwa mujibu wa Sheria ya Madini, Sura 123.
Akizungumza leo Novemba 25,2025 jijini Dodoma katika mkutano na waandishi wa habari, Mavunde amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha rasilimali madini zinawanufaisha Watanzania na kuimarisha usimamizi wa sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.
Mavunde amesema kuwa ongezeko la leseni zinazotolewa mwaka hadi mwaka ni ishara ya kuongezeka kwa uwekezaji kwenye sekta ya madini. Tangu mwaka 2021/2022 hadi Oktoba 2025, jumla ya leseni 48,673 zimetoa, sawa na utekelezaji wa asilimia 97.78 ya malengo.
Hata hivyo, licha ya mafanikio hayo, Mavunde amesema kuwa kumekuwapo na ukiukwaji wa masharti ya leseni kwa baadhi ya wamiliki. Makosa yanayorudiwa ni pamoja na kutokuendeleza maeneo ya leseni na kuyahodhi bila shughuli za utafiti au uchimbaji, kutolipa ada za leseni, kushindwa kutekeleza matakwa ya Local Content, kutotimiza wajibu wa Corporate Social Responsibility (CSR), pamoja na kushindwa kuthibitisha matumizi ya fedha kwenye uendelezaji wa leseni.
“Tume ya Madini ilitoa hati za makosa kwa leseni 205. Baadhi ya wamiliki walirekebisha makosa, lakini 44 wa leseni za utafutaji na 29 wa uchimbaji wa kati wameshindwa kufanya hivyo. Kwa hiyo naiagiza Tume ya Madini ifute leseni 73 ambazo hazijafanyiwa kazi,” amesema Mhe.Mavunde
Amesisitiza kuwa serikali haitowavumilia watu wanaohodhi leseni bila kuziendeleza, na kuielekeza Tume ya Madini kusimamia kikamilifu sheria kwa kutoa hati za makosa na kufuta leseni zote zisizotekelezwa bila upendeleo.
Aidha, Mavunde ametoa wito kwa wawekezaji wenye nia ya dhati wadogo kwa wakubwa kuwasilisha maombi ya leseni katika maeneo ya wazi, akiahidi kuwa wizara itahakikisha yanashughulikiwa kwa wakati.
Pia amewataka wamiliki wote wa leseni kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria, huku akiahidi kuwa serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wa ndani na nje wanaofanya uwekezaji wenye tija na unaochochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
