Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza na wakazi wa jiji la Dar es Salaam baada ya kukagua miundombinu ya umma pamoja na mali ambazo ziliathirika na vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amefanya ziara ya kukagua miundombinu hiyo leo Novemba 24, 2025 jijini Dar es Salaam.
…
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba ameagiza kurejeshwa kwa haraka kwa miundombinu ya umma katika Jiji la Dar es Salaam kufuatia vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa Serikali haitavumilia uzembe wala vitendo vinavyoathiri umoja wa kitaifa.
Katika ziara yake leo Novemba 24,2025 jijini humo, Dkt. Mwigulu alikagua mali na miundombinu ya umma iliyoharibiwa na vurugu hizo, akieleza kusikitishwa kwake na kiwango cha uharibifu kilichojitokeza. “Ni vigumu kuamini tukio kama hili limetokea Tanzania, nchi yenye amani,” amesema Dkt.Nchemba
Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameagiza kufutwa kwa sherehe za Uhuru za Desemba 9 mwaka huu na kuelekeza fedha zilizotengwa kwa ajili ya maadhimisho hayo kuelekezwa kwenye ukarabati wa miundombinu iliyoathiriwa. Dkt. Mwigulu amesema hatua hiyo inaonyesha dhamira ya Rais ya kurejesha hali ya kawaida na kulinda rasilimali za umma.
Dkt. Mwigulu amesisitiza umuhimu wa kutoa kipaumbele kwa wakandarasi wazawa katika kazi za ukarabati, akibainisha kuwa Watanzania wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi zinazotolewa hata kwa wakandarasi wa kigeni. “Tanzania ni ya Watanzania. Kazi ambayo Mtanzania anaweza kufanya, ifanywe na Mtanzania,” alisisitiza.
Ametoa onyo kali kwa watumishi wazembe na wala rushwa, akisema hawapaswi kuhamishwa bali kufukuzwa kazi. “Kuna vijana wengi wanaofanya kazi kwa bidii. Hatutavumilia uzembe wala rushwa,” alisema.
Aidha, Waziri Mkuu ametuma pole kwa wote walioathirika na vurugu hizo na amewataka Watanzania kuiunga mkono tume iliyoundwa na Rais kuchunguza tukio hilo ili hatua stahiki zichukuliwe.
Ameeleza kuwa wale wanaochochea uharibifu wa mali za umma wengi wao hawapo nchini na hawafahamu athari zinazowakumba wananchi. Amewaonya vijana kutokubali kutumiwa. “Mpenda Tanzania hawezi kukuambia uichome Tanzania. Kadri mnavyoiharibu, ndivyo wao wanavyonufaika zaidi,” alisema.
Ameongeza kuwa mara nyingi mataifa yenye rasilimali nyingi huandamwa na kuchochewa kwa vurugu, hivyo Tanzania—iliyojaaliwa gesi na madini—ina wajibu wa kuilinda miundombinu na umoja wake kwa nguvu zote.
Viongozi wa dini pia wametakiwa kuwa makini na jitihada zinazolenga kuwagawa wananchi, huku akisisitiza kuwa Rais Samia anaendelea kujenga misingi ya umoja na mshikamano nchini.
Dkt. Mwigulu amezielekeza Wizara ya Ujenzi, TANROADS, DART, UDART na TAMISEMI kushirikisha wadau mbalimbali ili ndani ya siku 10 shughuli jijini Dar es Salaam zirudi katika hali ya kawaida. Amesema mpango wa haraka wa marejesho uanzishwe wakati maandalizi ya mpango mpana yakiendelea.
“Wanaotushawishi kuchoma mali wanaturudisha kwenye umasikini,” alionya, akiwataka wananchi kulinda miundombinu ya Taifa na kukataa kushawishiwa kufanya vitendo vinavyochelewesha maendeleo.

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza na wakazi wa jiji la Dar es Salaam baada ya kukagua miundombinu ya umma pamoja na mali ambazo ziliathirika na vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amefanya ziara ya kukagua miundombinu hiyo leo Novemba 24, 2025 jijini Dar es Salaam.