Featured Kitaifa

SERIKALI KUONGEZA KONGANI ZA VIWANDA KUIMARISHA UZALISHAJI

Written by Alex Sonna

 

 

Serikali imepanga kuongeza maeneo maalum ya uwekezaji (kongani) nchini, hatua inayolenga kuchochea uzalishaji, kuongeza ajira na kuboresha mazingira ya kufanya biashara.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam alipotembelea Tume ya Ushindani (FCC), Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, alisema sekta ya viwanda imeendelea kukua na kuimarika, hususan katika uzalishaji wa malighafi unaochangia maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Waziri Kapinga alibainisha kuwa serikali inaendelea kupanua wigo wa viwanda ili kukuza ajira, kuongeza mapato ya ndani na kupanua mauzo ya nje kupitia utekelezaji wa sera endelevu zinazolenga kukuza sekta hiyo.

Aidha, alisema kuimarishwa kwa viwanda kutachochea ongezeko la uzalishaji wa malighafi, hatua itakayoongeza mapato na kuendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa wawekezaji na wajasiriamali.

Waziri huyo aliongeza kuwa sekta ya viwanda inaratibu shughuli za sekta mbalimbali, na kwamba serikali inaendelea kupunguza urasimu ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na wadau wa maendeleo.

Wakati huo Waziri  Kapinga, ametembelea Shirikisho la Viwanda Tanzania ambapo amesema maono ya Serikali kuelekea mwaka 2030 ni kuhakikisha kunaboreshwa uchumi wa viwanda, kuchochea ajira na kuimarisha maendeleo ya sekta ya viwanda nchini.

Mhe. Kapinga amesema Serikali itaendelea kudumisha ushirikiano mzuri na CTI, huku akibainisha kuwa mpango wa kuanzisha mitaa ya viwanda katika wilaya mbalimbali ni sehemu ya kuimarisha mchango wa sekta binafsi katika kukuza uchumi.

Ameeleza kuwa malengo ya Serikali ni kuongeza ajira, kupanua maeneo ya biashara, kuchangia ukuaji wa uchumi na Pato la Taifa, pamoja na kuongeza mauzo ya nje ili kufanikisha dhamira ya kufikia ajira milioni nane ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CTI, Leodeger Tenga, amesema shirikisho hilo limesisitiza umuhimu wa kuimarisha ukaribu na Wizara, na kutambua jitihada na mabadiliko yanayoendelea kufanywa na Serikali, huku akiahidi ushirikiano kwa manufaa ya sekta ya viwanda na uchumi wa Taifa.

]

About the author

Alex Sonna