Afisa Sheria Mwandamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Ramadhan Myonga akitoa wasilisho lake katika semina ya waandishi wa habari inayofanyika Jijini Dodoma.
Afisa Sheria Mwandamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Ramadhan Myonga akitoa wasilisho lake katika semina ya waandishi wa habari inayofanyika Jijini Dodoma.
Na Alex Sonna – DODOMA
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeisisitiza umuhimu wa kuimarisha ulinzi wa watumiaji wa huduma za kifedha nchini, ikibainisha kuwa hatua hiyo ni msingi muhimu wa uthabiti wa mifumo ya kifedha na kuhakikisha usawa katika soko.
Hayo yameelezwa leo Novemba 20,2025 na Afisa Sheria Mwandamizi wa BoT, Ramadhan Myonga,wakati akiwasilisha mada namna ya kumlinda mtumiaji wa huduma za fedha (SEMA NA BOT) , katika siku ya pili ya semina ya waandishi wa habari za uchumi na biashara inayoendelea jijini Dodoma.
Bw.Myonga, amesema ulinzi wa mteja ni muunganiko wa sheria, sera, taratibu na taasisi zinazolenga kuhakikisha haki za watumiaji zinalindwa, na kwamba watoa huduma wanatoa bidhaa kwa uwazi, usahihi na bila mbinu za udanganyifu.
“Kanuni za BoT za mwaka 2019 kuhusu Kumlinda Mtumiaji wa Huduma za Kifedha ndizo zinazoongoza ulinzi huo, kwa kuhakikisha watumiaji wanapata taarifa sahihi kabla ya kufanya maamuzi yoyote ya kifedha.”amesema Bw.Myonga
Amesema maboresho haya yametokana na mafunzo yaliyochangiwa na mgogoro wa kifedha wa mwaka 2007 hadi 2008, ambapo ilionekana wazi kwamba upungufu wa ulinzi wa wateja nchini Marekani ulikuwa miongoni mwa vichocheo vya kuvurugika kwa mifumo ya kifedha duniani.
Myonga amesema katika muktadha wa kimataifa, nchi nyingi zimechukua hatua za kisera na kisheria kuimarisha usimamizi wa masoko ya kifedha. Ameeleza kuwa Marekani ilipitisha Sheria ya Dodd–Frank mwaka 2010 na kuanzisha taasisi maalumu ya Consumer Financial Protection Bureau (CFPB) yenye jukumu la kumlinda mtumiaji wa huduma za kifedha.
Vilevile, Uingereza ilianzisha Financial Conduct Authority (FCA) mwaka 2012, iliyopewa dhamana ya kusimamia mwenendo wa soko na masuala ya haki za watumiaji. Myonga pia ametoa mfano wa nchi zinazoendelea, ikiwemo Zambia, ambazo zimefanya marekebisho ya sheria ili kuongeza masharti ya ulinzi kwa wateja wa huduma za kifedha.
Myonga amebainisha kuwa miongozo ya Umoja wa Mataifa kuhusu ulinzi wa watumiaji imeboreshwa, ikijumuisha maeneo muhimu yanayohusiana na sekta ya kifedha, ikiwa ni pamoja na uwazi, mwenendo wa biashara, ulinzi wa taarifa binafsi za wateja, elimu ya kifedha na utatuzi wa malalamiko. Miongozo hiyo imekuwa rejea muhimu kwa nchi zinazojitahidi kuimarisha uwajibikaji katika sekta ya fedha.
Akizungumzia hali ya Tanzania, Myonga amesema kuwa nchi inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kulinda watumiaji kwa kuimarisha usimamizi wa taarifa, kudhibiti mwenendo wa watoa huduma, kuendeleza elimu ya kifedha kwa wananchi, na kuhakikisha huduma zinatolewa bila unyanyasaji, udanganyifu au mbinu zisizo za haki.
“Hatua hizi zimekusudiwa kuongeza imani ya umma katika sekta ya fedha, kukuza ujumuishaji wa kifedha na kuhakikisha wananchi wanatumia huduma kwa usalama na uelewa sahihi,” amesema Myonga.