Ferdinand Shayo ,Arusha .
Benki ya NCBA imeshiriki zoezi la kupanda miti ya asili 11000 katika eneo la Olkokola Wilayani Arumeru Mkoani Arusha kwa kushirikiana na shirika la Kijani Pamoja kwa lengo la kuhakikisha uoto wa asili unarejea na kutimiza adhma ya Benki hiyo kupanda miti milioni 10 ifikapo mwaka 2030.
Akizungumza katika Zoezi la kupanda miti hiyo,Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NCBA Tanzania Alex Mziray amesema wamezindua mradi wa kupanda miti 11000 kwa lengo la kutunza mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho.
“Kwa kushirikiana na shirika la Kijani Pamoja wametupa njia ya kuhakikisha kuwa mradi huishii tu kwenye kupanda miti bali kuangalia jinsi ya kuendeleza miti na kuhakikisha inakua na hata ikifika miaka 10 ijayo uweze kuiona hiyo miti” Anaeleza Mziray.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kijani Pamoja Sarah Scott ameeleza furaha yake baada ya benki ya NCBA kuunga mkono mradi wa kupanda miti na kukuza miti na amekua akitumia mbinu ya “lipa ukue” inayolenga kuhamasisha wananchi kutunza miti huku wakijipatia kipato na tayari wataanza kupanda miti 11000 katika msimu huu wa mvua.
“Kupanda miti ni rahisi lakini kutunza miti iweze kukua ni ngumu sana lakini pia kupata miti sahihi na eneo sahihi kunasaidia kuleta matokeo chanya ya kuhakikisha kuwa tunarejesha uoto wa asili na mfumo wa ekolojia kwa ujumla” Alisema Sarah
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mwinyi Ahmed akizindua mradi huo kwa kupanda mti kama ishara ya uzinduzi amepongeza juhudi za benki ya NCB katika kutunza mazingira na kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabia ya nchi na kuwataka wadau wengine wa maendeleo kuiga mfano wa benki hiyo.
Mkuu wa Kitengo cha Mikakati Benki ya NCBA Tanzania Charles Mbatia amesema mpaka sasa wameshapanda miti 16000 ili kufikia lengo la kupanda miti milioni 10 ifikapo 2030.
Hata hivyo Mkuu wa Idara ya Mazingira Shirika la Kijani Pamoja ,Samwel Simon kazi yetu kubwa ni kuotesha miti ya asili kwenye maeneo yaliyoharibika ,vyanzo vya maji ,mito tukishirikiana na wadau mbali mbali kama ilivyo leo tumeshirikiana na benki ya NCBA.







