Meneja wa Idara ya Uendeshaji, Tawi la Benki Kuu Dodoma, Bw. Nolasco Maluli akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya waandishi wa habari Jijini Dodoma.

Meneja wa Idara ya Uendeshaji, Tawi la Benki Kuu Dodoma, Bw. Nolasco Maluli akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya waandishi wa habari Jijini Dodoma.

Meneja msaidizi uchumi wa Benki Kuu Tawi la Dodoma. Bw. Shamy Chamicha akiwasilishamada katika semina ya waandishi wa habari inayofanyika Jijini Dodoma.

Meneja Msaidizi wa Uhusiano wa Umma Benki Kuu ya Tanzania, Bi. Noves Moses akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya waandishi wa habari inayofanyika Jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna-DODOMA
Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imeanza semina maalum kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini, yenye lengo la kuwajengea uwezo juu ya majukumu, mifumo na huduma za benki hiyo pamoja na masuala mapana ya uchumi na fedha.
Semina hiyo ya siku tatu imefunguliwa leo Novemba 19,2025 jjijini Dodoma na Meneja wa Idara ya Uendeshaji, Tawi la Benki Kuu Dodoma, Bw. Nolasco Maluli, amesema mpango huo ni muhimu katika kuongeza uelewa wa waandishi juu ya masuala ya fedha na uchumi, ili waweze kuandika habari sahihi na zenye weledi zinazowasaidia wananchi.
Semina hiyo inaratibiwa na BOT kwa waandishi wa habari kutoka Mikoa mitano ikiwemo Dodoma,Morogoro,Pwani,Dar es Salaam na Zanzibar
Bwana Maluli amesema kuwa semina hiyo inalenga kukuza uelewa wa waandishi kuhusu majukumu na huduma zinazotolewa na BOT. Aliongeza kuwa itawapatia waandishi ufahamu wa kina kuhusu masuala ya fedha, ikiwemo sera za fedha na mifumo ya malipo.
“BOT imekuwa ikipata mafanikio kupitia ushirikiano na vyombo vya habari, ikiwamo kuongezeka kwa weledi katika habari na makala za uchumi, upatikanaji wa ufafanuzi sahihi wa masuala ya kifedha kwa umma na kuimarika kwa mahusiano kati ya BOT na wanahabari.”amesema Bw.Maluli
Akizungumzia matarajio ya benki hiyo, Bwana Maluli amesema BOT inatarajia kuona waandishi wa habari wakiandika habari za uchumi na fedha kwa usahihi zaidi, pamoja na kutoa maoni yenye kuchochea maboresho katika mifumo ya fedha na malipo ili kuboresha huduma kwa wananchi.
Miongoni mwa mada zitakazojadiliwa katika semina hiyo ni Muundo na Majukumu ya BOT, Sera ya Fedha Inayotumia Riba, Elimu Kuhusu Hati Fungani, Elimu ya Fedha na Usajili wa Vikundi, Ulinzi na Huduma za Kifedha, Usimamizi wa Mifumo ya Malipo, pamoja na Alama za Usalama katika Noti za Tanzania.
Semina hiyo inaendelea jijini Dodoma na inatarajiwa kuongeza uwezo wa waandishi wa habari katika kuripoti masuala ya uchumi na fedha kwa namna itakayowasaidia wananchi kupata taarifa sahihi na zenye manufaa.