Featured Kitaifa

TTCL  YAENDELEA KUKUA KIDIGITALI,YAZINDUA ‘T-FIBER TRIPLE HUB’

Written by Alex Sonna

 

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) linaendelea na safari ya kuboresha na kuimarisha mawasiliano ya kidijitali nchini ambapo limezindua huduma mpya ya Faiba Mlangoni Kwako iitwayo ‘T-fiber Triple Hub’ ikiwa ni kifurushi kipya kilichobuniwa kwa kuzingatia mahitaji ya kizazi cha kidijitali cha leo.

Huduma hiyo imezinduliwa leo Novemba 12, 2025 jijini Dar es Salaam na Meneja wa Masoko wa TTCL, Bi. Janeth Maeda ambaye ameeleza kuwa, dunia ya sasa inaendeshwa na teknolojia, hivyo TTCL imewekeza kwa nguvu kuhakikisha Watanzania wanapata huduma za mawasiliano zenye kasi, ubora na gharama nafuu.

“Kifurushi hiki ni cha kipekee kwani kinaunganisha huduma tatu muhimu ikiwemo Intaneti ya kasi isiyo na kikomo, huduma ya simu ya mezani (Voice Service), huduma ya intaneti pamoja na dakika kwa simu ya mkononi”, amesema Bi. Janeth.

Amefafanua kuwa, lengo la huduma hiyo mpya ni kurahisisha maisha ya Watanzania kwa kuwapa huduma zote muhimu kwa kifurushi kimoja na bili moja ambapo huduma hiyo inalenga familia, biashara ndogo na kubwa, pamoja na taasisi zinazohitaji mawasiliano ya uhakika na yenye thamani halisi.

Akielezea kuhusu gharama, Bi. Janeth amesema zinaanzia shilingi 70,000 kwa mwezi ambapo wateja wa T-Fiber Triple Hub watapata intaneti ya kasi hadi 20 Mbps (upload na download), dakika 300 za mawasiliano ya mezani, pamoja na GB 20 kwa matumizi ya simu ya mkononi.

Amesisitiza kuwa kifurushi hicho kinatoa urahisi wa kipekee kwani mteja anaweza kufurahia huduma tatu kwa pamoja popote alipo, kupitia miundombinu imara ya TTCL.

Uzinduzi wa T-Fiber Triple Hub ni ishara ya mageuzi mapya katika mawasiliano ya kidijitali nchini Tanzania. Huduma hiyo ni sehemu ya juhudi za shirika kuunga mkono ajenda ya serikali ya kutanua wigo wa matumizi ya TEHAMA na kuunganisha Watanzania wote katika mfumo wa kidijitali.

About the author

Alex Sonna