RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi, amezuru na kusoma dua katika kaburi la Al-Habib Ahmad bin Abubakar bin Sumeit, aliyekuwa mwanazuoni mkubwa wa fani mbalimbali za dini ya Kiislamu na aliwahi kuwa Kadhi Mkuu wa Zanzibar kati ya mwaka 1883 hadi 1886.
Amesema ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha Tanzania na Zanzibar zinaendelea kuwa visiwa vya amani, umoja na mshikamano, ili kuwezesha utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa mafanikio.
“Tuendelee kuiombea nchi yetu amani, kwani bila amani hakuna maendeleo. Serikali inatekeleza mipango mingi ya maendeleo, hivyo tunapaswa kuiombea Mungu atujaalie utulivu na mshikamano,” amesema Dk. Mwinyi.
Alhaj Dk. Mwinyi amewataka viongozi wa dini kuendeleza juhudi za kuhimiza maadili mema, upendo na mshikamano miongoni mwa wananchi, ili kuijenga jamii yenye maadili na inayomcha Mungu.
