Featured Kitaifa

PROF. MUSHI: ELIMU YA JUU NI INJINI YA MAENDELEO YA TAIFA

Written by Alex Sonna

Na.Mwandishi Wetu

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi, amesema Serikali imejipanga kwa dhati kuimarisha elimu ya juu nchini ili kuongeza ubora wa taaluma na tafiti zinazotekelezwa katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu.

Akizungumza jijini Dodoma leo, Novemba 7, 2025, wakati wa kikao kazi na viongozi kutoka vyuo vikuu na taasisi mbalimbali za elimu ya juu, Prof. Mushi amesema  Serikali inaendelea kuweka mikakati thabiti ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, pamoja na kuongeza ufanisi wa utendaji katika sekta hiyo.

Amesema hatua kadhaa zimeanza kuchukuliwa, ikiwemo kuongeza nafasi za mafunzo ya uzamili na uzamivu kwa watumishi wa vyuo, kuimarisha motisha na masilahi, sambamba na kukuza uwezo wa kufanya tafiti zenye tija kwa maendeleo ya taifa.

“Serikali inatambua kuwa elimu ya juu ndiyo injini ya maendeleo, hivyo tutaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo kuhakikisha tunaboresha miundombinu, tafiti na ubora wa wahitimu wetu,” amesema Prof. Mushi.

Hata hivyo ameongeza kuwa wizara itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha watafiti na wahadhiri kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi, kwa manufaa ya taifa na kizazi kijacho.

About the author

Alex Sonna