Featured Kitaifa

HIFADHI YA MPANGA-KIPENGERE YAENDELEA KUWA LULU YA VIZAZI VIJAVYO

Written by Alex Sonna
Na Beatus Maganja, Njombe.
Wahenga walioshiba tunu za uhifadhi na utalii nchini waliwahi kusema “Kama unataka kujua uzuri wa Tanzania tembea ndani ya moyo wake, na moyo huo ni Hifadhi zake”. Wengine walisema “Kuna safari ambazo hubadilisha mawazo, na kuna nyingine zinazogusa mwili, nafsi, moyo na roho”.

Kuna mahali duniani ambapo miamba huzungumza Kwa sauti ya utulivu, mito ikiimba nyimbo za kale na upepo ukiandika mashairi yasiyofutika juu ya majani ya kijani, mahali ambapo asili huvaa vazi za kizalendo, mahali ambapo historia ikiishi, elimu ikitembea na Tanzania ikitabasamu. Hapa ndipo unapoikuta Hifadhi ya Mpanga-Kipengere, hifadhi iliyopo Mikoa ya Mbeya na Njombe ikiwa chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA.
Leo Novemba 7, 2025 TAWA tulishuhudia ukurasa mwingine mzuri wa historia ya elimu na uhifadhi ulioandikwa ndani ya Hifadhi hii, wakati walimu na wanafunzi wa shule ya Sekondari Lupalilo kutoka Mkoa wa Njombe walipoitembelea Kwa ziara ya kujifunza na kutalii.
Ziara hii si safari ya kawaida, bali mwendelezo wa hamasa inayofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia TAWA inayosisitiza dhana ya “Tumerithishwa Tuwarithishe” lakini pia dhana ya “Tembea Tanzania, Jifunze Tanzania” dhana za utalii wa ndani zilizovuka mipaka ya starehe na kuwa chombo cha elimu, uchumi na uzalendo.
Kwa miaka kadhaa sasa, Shule ya Lupalilo imekuwa mfano wa Kuigwa Kwa kuleta wanafunzi Mpanga-Kipengere, Si Kwa kutazama tu mandhari yake, bali kujifunza Kwa macho, miguu na akili. Mahali ambapo kila mwamba ni somo, kila korongo ni darasa na kila chemichemi ni nukuu ya uumbaji.
Ni Hifadhi pekee nchini ambapo mwanafunzi huweza kushuhudia miamba yote mitatu ya sayansi ya jiolojia. Mwamba moto, mwamba tabaka na mwamba geu.
Lakini Mpanga-Kipengere haizungumzi tu jiolojia, bali ni kitovu cha urithi wa historia ya Tanzania, mahali ambapo bado yanapumua majina makubwa ya Chifu Mkwawa Mkwavinyika na Chifu Merere, mashujaa waliotetea ardhi hii kabla haijawa hifadhi wakiamini kuwa nchi bila heshima ya ardhi yake ni nyumba isiyo na msingi.
Kupitia ziara kama hizi, vijana wanajengewa moyo wa uzalendo, kupenda mazingira na kuthamini rasilimali za taifa. Ni mahali ambapo vizazi vinalelewa si tu kuwa wasomi, bali walinzi wa urithi wa Tanzania.
Kwa maneno mafupi, Hifadhi ya Mpanga-Kipengere ni darasa liliandikwa Kwa mikono ya Muumba mwenyewe, ni darasa la uhai,mahali ambapo kila mgeni huondoka na zawadi inayoonekana Kwa macho ya nyama, zawadi ya kutua msongo wa mawazo na kuongeza upendo Kwa nchi yake, mahali ambapo mgeni huondoka akiwa amebeba zaidi ya kumbukumbu na ndoto mpya, ndoto ya kizazi kinachotambua kuwa utalii ni darasa, na uhifadhi ni urithi.

About the author

Alex Sonna