Featured Michezo

YANGA YAHAMIA ZANZIBAR  MECHI ZA MAKUNDI LIGI YA MABINGWA AFRIKA

Written by Alex Sonna

KLABU ya Yanga imetangaza rasmi kwamba mechi zake za nyumbani katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu zitachezwa katika Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, amesema kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya tathmini ya kina kwa kuzingatia maslahi mapana ya klabu.

Yanga, ambayo imepangwa Kundi B pamoja   na vigogo wa Afrika Kaskazini ambazo ni Al Ahly ya Misri, JS Kabylie ya Algeria na AS FAR ya Morocco imeamua kuhamishia michezo hiyo visiwani humo, baada ya kutumia Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, katika mechi za awali dhidi ya Wiliete ya Angola na Silver Strikers kutoka Malawi.

“Baada ya kufanyika tathmini ya kina na kwa maslahi mapana ya klabu yetu, napenda kuwatangazia kwamba mechi za Yanga katika hatua ya makundi zitafanyika katika kisiwa cha Unguja kwenye Uwanja wa New Amaan Complex,” amesema Kamwe.

“Nichukue fursa hii kuwaomba mashabiki na wanachama wa Yanga katika visiwa vya Pemba na Unguja kuanza maandalizi ya haraka kuhakikisha tunafanya vizuri.”ameongeza

Wakati huo huo, ameelezwa kuwa Yanga itaendelea kutumia Uwanja wa KMC Complex kwa michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano mengine ya ndani.

Uamuzi huo unaifanya Yanga kuwa klabu ya tatu kutoka Tanzania Bara kutumia Uwanja wa New Amaan Complex kwa mechi za mashindano ya Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) msimu huu, baada ya Singida Black Stars na Azam FC zinazoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

About the author

Alex Sonna