MSHAMBULIAJI wa Yanga, Clement Mzize, amefanyiwa upasuaji wa goti na anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha kati ya wiki nane hadi kumi, sawa na takribani miezi miwili, hali inayomfanya kuukosa mfululizo wa mechi muhimu ikiwemo Dabi ya Kariakoo na michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi dhidi ya timu za Afrika Kaskazini.
Akithibitisha taarifa hizo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, amesema baada ya mshambuliaji huyo kutonesha jeraha lililomuweka nje kwa wiki tatu awali, uongozi wa klabu ulilazimika kuridhia kufanyika kwa upasuaji huo kwa ushauri wa madaktari.
Mzize, ambaye alikuwa kinara wa mabao kwa wachezaji wazawa katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita baada ya kufunga mabao 14, alipata majeraha hayo wakati Yanga ikiichapa Wiliete SC ya Angola mabao 3-0 kwenye mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa Septemba 19, 2025.
“Ni kweli Mzize amefanyiwa upasuaji wa goti, na kwa mujibu wa daktari atakuwa nje ya uwanja kwa wiki nane hadi kumi, hivyo hatutakuwa na huduma ya mchezaji huyo kwa muda huo,” amesema Kamwe.
Aidha ameongeza kuwa hatua hiyo imefuata uchunguzi wa kina na vipimo vilivyobainisha umuhimu wa upasuaji huo.
“Upasuaji huo umezingatia vipimo vikubwa alivyofanyiwa. Haikuwa rahisi kwa mchezaji kukubaliana na uamuzi huo, lakini kwa msaada wa wanasaikolojia na madaktari bingwa, ilichukua siku tatu kumshawishi na kufanikisha hatua hiyo,” amesema Kamwe.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu, Mzize ataendelea na programu maalum ya mazoezi ya kurejesha mwili taratibu chini ya usimamizi wa benchi la tiba la Yanga hadi atakaporuhusiwa kurejea uwanjani.