Featured Michezo

MKUU WA JKT ATOA WITO KWA WATANZANIA KUIUNGA MKONO JKT QUEENS LIGI YA MABINGWA AFRIKA

Written by Alex Sonna


Na Mwandishi Wetu

MKUU wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele, amewataka Watanzania kuiunga mkono timu ya JKT Queens, ambayo itaiwakilisha Tanzania na Ukanda wa CECAFA katika michuano ya Ligi ya Mabingwa  Afrika kwa upande wa  wanawake.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa droo ya upangaji wa makundi iliyofanyika mjini Cairo, Misri,leo Oktoba 27, 2025, Meja Jenerali Mabele amesema  JKT Queens imepangwa Kundi B pamoja na bingwa mtetezi TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Asec Mimosas kutoka Ivory Coast, na Gaborone United kutoka Botswana.

Michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake inatarajiwa kuanza kutimua vumbi kuanzia Novemba 8 hadi 21, 2025.

Meja Jenerali Mabele ametoa wito kwa Watanzania kushikamana na kuishangilia timu hiyo ya kijeshi yenye wachezaji wazawa, akisisitiza kuwa JKT Queens inahitaji sapoti ya kitaifa kama ile inayotolewa kwa klabu kongwe za Simba na Yanga zinapowakilisha nchi kimataifa.

“JKT Queens ni timu ya kizalendo, inawakilisha siyo tu JKT bali Taifa zima. Tunapaswa kuwaunga mkono kwa nguvu zote ili waweze kufanya vizuri na kuleta heshima kwa Tanzania,” amesema  Meja Jenerali Mabele.

Kwa upande wake, Mratibu wa timu hiyo, Meja Ester Ryoba, amesema maandalizi ya timu yako yamekamilika na wachezaji wapo katika hali nzuri.

“Tumejiandaa vizuri kwa ajili ya michuano hii. Wachezaji wako kwenye morali ya hali ya juu na dhamira yetu ni moja tu kurejea nyumbani na ubingwa wa Afrika,” amesema  Meja Ryoba.

JKT Queens, ambayo inashiriki michuano hiyo kwa mara ya pili, itakuwa miongoni mwa timu nane bora za wanawake barani Afrika zitakazowania taji hilo lenye hadhi kubwa katika soka la wanawake.

About the author

Alex Sonna