Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Katika jitihada za kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa kisiwa cha amani, viongozi wa dini kutoka mikoa ya Dodoma na Singida wamekutana jijini Dodoma katika kongamano la kuliombea taifa amani na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Kongamano hilo limefanyika leo Jijini Dodoma Oktoba 25,2025 likiongozwa kwa kaulimbiu isemayo “Amani na Utulivu ni Jukumu Letu” ambapo limewakutanisha viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali walioungana kwa sauti moja ,kuhimiza wananchi kudumisha amani katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.
Akizungumza katika kongamano hilo Shekhe wa Mkoa wa Dodoma na mwenyekiti wa kamati ya maridhiano ya viongozi wa dini mbalimbali mkoa wa Dodoma Alhaj Dkt. Rajab Mustafa Shabani ambapo amesitiza umuhimu wa Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchaguzi kwa amani, huku akipinga vikali wito wa maandamano yanayoweza kuvuruga utulivu wa taifa.
”sisi kama watanzania tunatakiwa kuwa watiifu wa maelekezo yanayotolewa na viongozi wa serikali na dini,kuwatii wenye mamlaka siyo agizo letu viongozi wa dini ni agizo kutoka kwa mungu.
”Oktoba 29 hakuna maandamano ya kuvuruga amani bali kuna maandamano ya kwenda kupiga kura na tumekua tukisikia mheshimiwa Rais Samia akiwataka watanzania wajitokeze kwa wingi kupiga kura,tusiwe sehemu ya vurugu, maandamano au maneno ya kuchochea chuki amani ikipotea, wote tunateseka,” amesema.

Shekhe huyo pia amewahimiza viongozi wa dini kutumia nafasi zao kuhubiri amani na mshikamano badala ya kugawanya waumini kwa misingi ya kisiasa.
Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Karmeli Assemblies of God (KAG), Dkt. Evans Chande amesema elimu inapaswa kutolewa kwa vijana kutokana na kutumika mara nyingi kwenye vurugu.
“Sisi tukae na vijana, tuwaambie kwamba jamani msije mkaitumbukiza nchi hii kwenye matatizo mjue ya kwamba hatutakuwa na mahali pa kwenda, watakaothirika watoto, wazee, walemavu hao ndiyo wataathirika na wajawazito, kwahiyo tukae na makundi haya lakini pia vilevile hata wakuu wa taasisi mbalimbali tukae nao tuwashauri,”amesema.
Sanjari na hayo Askofu Chande amegusia suala la uadilifu kwani kuna watu ambao hawafanyi vizuri katika eneo hilo kwenye ofisi zao na kuitia doa Serikali kisha kuonekana haifanyi vyema.
Kwa upande wake, Shekhe wa Mkoa wa Singida, Issa Nasoro alitoa ametoa wito kwa viongozi wa dini kujitathmini na kuepuka kuwa chanzo cha migawanyiko katika jamii.
“Kumekuwa na tabia ya baadhi ya viongozi wa dini kujiingiza kwenye maneno ya kisiasa na kuilaumu serikali kwa mambo ambayo wao wenyewe wanachangia kuyafanya tumeshuhudia siku za hivi karibuni viongozi wa dini wakijiteka wenyewe na kusingizia serikali,hivyo turejee kwenye misingi ya imani ya upendo, ukweli na amani,” amesema.
Kongamano hilo, limejumuisha viongozi wa Kiislamu, Kikristo na madhehebu mengine, liliambatana na maombi maalum kwa ajili ya taifa, likiwa na ujumbe wa umoja na mshikamano bila kujali tofauti za imani au itikadi za kisiasa.
Wakizungumza kwa pamoja, viongozi hao walikubaliana kuwa uchaguzi ni tukio la kidemokrasia, si vita, na hivyo wananchi wanapaswa kutambua kuwa amani ndiyo urithi mkubwa wa taifa.
“Tunapaswa kuilinda amani kama tunavyolinda maisha yetu. Bila amani, hakuna ibada, hakuna biashara, hakuna maendeleo,” amesema mmoja wa washiriki wa kongamano hilo.
Kongamano hilo limeibua matumaini mapya kwamba viongozi wa dini wataendelea kuwa nguzo muhimu katika kudumisha amani na umoja wa kitaifa wakati huu wa kuelekea uchaguzi.