Featured Kitaifa

REA YAANZA KUSAMBAZA MITUNGI YA GESI 19,530 MKOANI MARA

Written by Alex Sonna

 

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeanza kusambaza mitungi ya gesi 19,530 yenye thamani ya Shilingi milioni 390 katika wilaya sita za mkoa wa Mara ambapo mradi huo utawanufasiha wakazi wa maeneo ya vijijini.

Akizundua mradi huo leo, tarehe 21 Oktoba, 2025 kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Mara Kanali, Evans Mtambi, Mkuu wa wilaya ya Musoma, Mhe. Juma Chikoka amesema Serikali imeweka ruzuku kupunguza gharama ili Wananchi wajaribu matumizi ya nishati hiyo na kuona faida yake ikilinganishwa na matumizi ya kuni na mkaa.

Mhe. Chikoka amesema Mradi huo wa REA ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini huku Wananchi mkoani humo wakiiomba seijali kusogeza vituo vya kujaza gesi karibu na makazi yao.

Mitungi hiyo yenye ujazo wa kilo 6 kila moja itauzwa kwa bei ya ruzuku ili kuwezesha Wananchi wa maeneo hayo ya vijijini kuanza matumizi ya nishati hiyo na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa ambayo yameelezwa kuwa na athari nyingi ikiwemo za kiafya na kimazingira.

Chikoka amesema mitungi hiyo inatarajiwa kusambazwa katika wilaya zote sita (6) za mkoa wa Mara na kueleza kuwa Serikali inatambua athari zinazowakumba Wananchi hasa Wanawake kutokana na matumizi ya kuni na mkaa.

“Serikali inatambua changamoto zinazotokana na matumizi ya kuni na mkaa ukiachana na hili la mabadiliko ya tabia nchi lakini pia kuna suala la afya hivyo ikaona ipo haja ya kuja na mradi huu kwa maslahi mapana ya watu wake,” amesema

Chikoka amewataka wakazi wa mkoa huo kutumia fursa hiyo ili kuweza kujipatia mitungi hiyo na kuanza safari ya matumizi ya nishati ya gesi katika mapishi yao ya kila siku.

Rais Samia Suluhu Hassan tayari alitangaza mkakati wa Serikali wa kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini hadi kufika asilimia 80 mwaka 2034.

Chikoka amesema jamii inapaswa kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia kwenye nishati safi ya kupikia kwa maelezo kuwa mbali na faida za kiafya na mazingira pia matumizi ya nishati safi ni gharama nafuu ikilinganishwa na kuni na mkaa.

Akitoa taarifa ya mradi huo katika kijiji cha Etaro wilayani Musoma leo Oktoba 21,2025, Mhandisi wa Miradi kutoka REA, Geofrey Gedo amesema kuwa kwa mujibu wa utafiti waathirika wengi wa matumizi ya nishati isiyokuwa salama ni Wanawake na Watoto jambo ambalo Serikali imeona ipo haja ya kulitafutia ufumbuzi wa kudumu.

“Utafiti uliofanywa mwaka 2016 ulibainisha kuwa watu 33,024 hufarki nchini kila mwaka kabla ya wakati hii ni sawa na asilimia 8.49 ya vifo vyote nchini na vifo hivi hutokana na magonjwa ambayo yanachangiwa na uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba huku waathirika wengi wakiwa ni Wanawake na Watoto,” amesema.

About the author

Alex Sonna