Featured Kitaifa

MIRADI YA KIMKAKATI YA TANROADS INAUFUNGUA MKOA WA SONGWE-ENG BISHANGA

Written by Alex Sonna

Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo upanuzi wa barabara kuu ya TANZAM kipande cha Igawa – Tunduma (Km 218) na Ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja wa magari katika barabara hiyo eneo la Iboya Mkoani Songwe.

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita Mkoa wa Songwe ulikumbwa na changamoto kwenye baadhi ya Barabara kutokana na mvua za El-Nino katika Barabara ya Kamsamba inayounganisha mkoa huo na mkoa jirani wa Rukwa ambapo Bilioni 32 zilitolewa ili kuondoa changamoto ya maeneo yaliyoathiriwa na mvua za El-Nino ikihusisha Daraja la Mpapa lenye urefu wa mita 60 katika barabara ya Mlowo – Kamsamba kwa shilingi bilioni 7, Daraja la Sange lenye mita 25 na barabara za maingilio kwa gharama ya Shilingi Bilioni 7.3, daraja la Kabalisi lenye urefu wa mita 40 na barabara za maingilio kwa gharama ya Shilingi Bilioni 7.7, na Ujenzi wa barabara ya Zege na kuchoronga milima kwa gharama ya Shilingi Bilioni 8.8 ambapo mradi unatakelezwa na makandarasi wazawa ukiwa umefikia takribani asilimia 90 mpaka sasa.

Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe Mhandisi Suleiman Bishanga amesema hayo tarehe 18 Octoba 2025 wakati akizungumza ofisini kwake kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita katika sekta ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja.

Amesema kuwa mkoa wa Songwe una mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 1,034.71 ambapo kati ya hizo kilomita 257 ni Barabara za lami na Kilomita 810 ni barabara za changarawe, Amesema serikali imekamilisha ujenzi wa daraja la Kamsamba lenye urefu wa mita 84 kwa gharama ya shilingi bilioni 17 na Daraja la Mpapa/Mkonko lenye urefu wa mita 60 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 7 ambalo limefikia asilimia 90 likiwa linajengwa na mkandarasi mzawa ABEMULO.

Mhandisi Bishanga amesema kuwa serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ya Ibungu – Kafafa inayojengwa kwa sehemu mbili zilizoathirika za madaraja na sehemu zenye maporomoko makubwa ambazo ni ujenzi wa Daraja katika eneo la Sange wilaya ya Ileje linajengwa na mkandarasi mzawa GEMEN likiwa limefikia asilimia 92 kwa gharama ya shilingi Bilioni 7.7 na sehemu ya pili ni ujenzi wa Daraja la Kabalisi linalojengwa na mkandarasi mzawa JASCO kwa gharama ya shilingi Bilioni 7.7

Amesema kuwa serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ya Ndembo Kwenda Ngana inayounganisha mkoa wa Songwe na Mkoa wa Mbeya katika mpaka wa Kasumulo nchini Malawi unaojengwa na mkandarasi mzawa MBUYA kwa gharama ya Shilingi Bilioni 8, pia kazi ya kurekebisha maporomoko ya udongo (Landslide) katika maeneo ya milima inaendelea na mkandarasi huyo mzawa na mradi umefikia asilimia 85.

Mhandisi Bishanga amesema kuwa zaidi ya Bilioni 300 zimetumika katika mkoa huo ikiwemo ujenzi wa kilomita 50 za lami katika barabara ya Mpemba – Isongole mradi ambao umekamilika kwa asilimia 100 na zaidi ya Bilioni 107 zimetumika. “Kwenye mradi huo limejengwa daraja kubwa katika mto Songwe linalounganisha nchi ya Tanzania na Malawi kupitia wilaya ya Ileje kwenye mpaka wa Isongole. Kuanzia katika eneo la Isongole zimetolewa Bilioni 74 kutekeleza mradi wa Barabara ya Isongole II – Ndembo – Ngana/Isoko na mkandarasi amefikia asilimia 7.5” Amesisitiza Mhandisi Bishanga

Mhandisi Bishanga ameeleza kuwa mradi mwingine ni wa ujenzi wa barabara ya Igawa – Tunduma (km 218) na Uyole – Songwe (Bypass) km 48.9 (PPP) Contract ambao ni moja ya mikakati endelevu ya Serikali ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nyanda za juu kusini na Nchi za kusini mwa Afrika, Mfano. Zambia, DRC n.k kwa kuboresha miundombinu ya barabara ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji. Mradi huu unatekelezwa kwa mfumo wa ubia wa Serikali na Sekta binafsi yaani PPP (Public, Private, Partership).

Hata hivyo amebainisha kuwa serikali inaendelea na Ujenzi wa Barabara ya Kamsamba – Mlowo kilomita 130 kwa awamu ya kwanza Mlowo – Zelezeta (Lot 1) Km 5 kwa kiwango cha lami na kutoka Kamsamba – Mkonko kilomita 5 zitaanza kujengwa na tayari mkandarasi yupo katika hatua za mwisho ili kuanza kazi haraka kwa mujibu wa mkataba.

About the author

Alex Sonna