Na Meleka Kulwa, Dodoma
Mgombea ubunge wa Jimbo la Mtumba kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Anthony Mavunde, ameahidi kuimarisha sekta ya usafirishaji ndani ya jimbo hilo kwa kuboresha mazingira ya kazi ya waendesha bodaboda na bajaji.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Viwanja vya Tambukareli, jijini Dodoma, Oktoba 18, 2025, Mavunde amesema atashirikiana na viongozi wa vituo vya usafirishaji, Jeshi la Polisi na mgambo wa jiji kuhakikisha usumbufu kwa waendesha bodaboda na bajaji unapungua.
Aidha, ameahidi kujenga mabanda ya kivuli katika vituo vyote vya bodaboda na bajaji ndani ya Jimbo la Mtumba kuanzia mwezi Novemba mwaka huu, ili kuboresha mazingira ya kazi kwa watoa huduma hao.
Mavunde pia amesema ataweka mpango maalumu utakaowawezesha waendesha bodaboda kumiliki pikipiki zao badala ya kutumia za mikataba, mpango ambao atasimamia yeye binafsi.
Katika kuunga mkono juhudi hizo, Mavunde amechangia shilingi milioni 10 kwenye mfuko wa maafisa usafirishaji, na kufanya mfuko huo kufikia jumla ya shilingi milioni 20.
“Amekumbusha kuwa awali aliwahi kuchangia kiasi kama hicho wakati wa ufunguzi wa Ofisi za Maafisa Usafirishaji Mkoa wa Dodoma, na kuweka mpango wa kusaidia waendesha bodaboda kununua matairi mapya kwa malipo ya awamu kati ya shilingi 8,000 hadi 10,000.”amesema
Ameongeza kuwa ataendelea kushirikiana na wadau wa sekta hiyo kuhakikisha changamoto mbalimbali za usafirishaji zinatatuliwa, sambamba na kusisitiza umuhimu wa amani na ushiriki wa wananchi katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Akizungumzia maendeleo ya miundombinu ya Ofisi za Maafisa Usafirishaji Mkoa wa Dodoma, Mavunde amesema Dodoma ni miongoni mwa mikoa michache yenye ofisi bora zilizojengwa kwa juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan huku akibainisha kuwa ofisi hizo zimeboreshwa kwa kujengwa uzio na kuwezeshwa miundombinu ya kisasa ya kufanyia kazi.
Mavunde amewashukuru maafisa usafirishaji, waendesha bodaboda na bajaji kwa ushirikiano waliomuonesha katika kipindi cha utumishi wake kama Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini,huku akisema wamekuwa sehemu muhimu katika maendeleo ya sekta ya usafirishaji.
Vilevile, amewahimiza wananchi wa Jimbo la Mtumba kujitokeza kwa wingi tarehe 29 Oktoba kupiga kura kwa wagombea wa CCM katika ngazi zote, akiwemo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani.