Chunya
Katikati ya mapori ya Itumbi- Chunya ambako ardhi inaongea kwa dhahabu, kuna kikundi cha watu wasio maarufu sana – lakini kazi yao ni ya thamani kuliko dhahabu yenyewe. Hawa ni Wakaguzi wa Migodini na Wafunga Matimba, kundi la watu 160 waliotoa maisha yao kulinda usalama wa wachimbaji Wadogo.
Dominick Nchimbi Katibu wa Kikundi hicho anasema kila siku asubuhi wanakikundi huvaa buti, kofia ngumu na kubeba daftari dogo la kumbukumbu, wanaheshimiwa na wachimbaji kama macho ya pili ya migodi na wanapoulizwa siri ya kazi yao, anasema kwa ‘’utulivu, uzoefu unatusaidia kunusa hatari kabla ya chochote kutokea,’’ wakiongozwa na kaulimbiu yao, “Usalama Kwanza, Kazi Baadaye”.
Anasema uzoefu huo umesaidia kuepusha ajali nyingi. Kwa macho ya kawaida, migodi inaonekana mashimo tu. Lakini kwao, ni vitabu vilivyofunguka vya usalama – vyenye kurasa za mafunzo, onyo, na matumaini.
Wakaguzi hawa, wanaotambuliwa na Ofisi ya Madini, hushirikiana na maafisa ukaguzi kutoka Ofisi ya Madini huzunguka maduara ya wachimbaji wakichunguza mikondo ya hewa, miamba inayosogea, na njia za dharura. Wanapobaini hatari, hawangoji ajali – wanatoa taarifa mapema, wakipendekeza hatua. Wamekuwa daraja si la saruji, bali la mawasiliano na kati ya Serikali na wachimbaji.
Lakini kazi yao haiishii kwenye ukaguzi. Wanapofunga matimba, nyaya na nguzo zinazodhibiti miamba isiyokaa sawa, wanafunga pia matumaini ya familia nyingi. Wanaweka uhai salama kwa kila pigo la nyundo linalogonga mwamba.
Na hapa ndipo hadithi ya Chunya inabadilika. Zamani, dhahabu ilionekana kama kazi ya kuchimba tu. Leo, kupitia vikundi kama hicho, Sekta ya Madini inapanuka. Si wachimbaji tu ni pia wakaguzi, mafundi wa vifaa vya usalama, walimu wa mazingira, wataalamu wa kijamii wote wanapata ajira.
Chunya ya leo haichimbi tu – inachimba kwa kufuata kanuni na dhahabu haifiki sokoni kwa miujiza inapita kwa kusajiliwa kwenye rejesta yaani kitabu maalum kwenye mwalo.
Hawa ni mashahidi wa usalama, kwa taratibu zilizowekwa. Katika macho ya wengi, hawa ni watu wa kawaida. Lakini kwa wachimbaji wa Chunya, wakaguzi wa migodi na wafunga matimba ni mashujaa wa kimya – wanaoona fursa kwa jicho la kipekee, wanaochimba kwa akili kabla ya kutumia nguvu.
Hawa pia wanatumika maeneo mbalimbali kukiwa na migogoro kati ya wamiliki wa duara kwa kushirikiana na maafisa madini, hushuka na kuangalia hali halisi kule chini na inasaidia kufanya maamuzi ukiwa saiti.
Kila siku, Sekta ya Madini inaendelea kuzalisha ajira mpya – nyingine zikiwa za kimya kimya, lakini zenye mchango mkubwa kwa familia na taifa. Si wachimbaji tu, bali pia wakaguzi, mafundi, walimu na washauri wa usalama – wote ni sehemu ya mnyororo wa thamani unaoinua maisha.
Hii ndiyo hadithi ya Chunya – dhahabu inayochimbwa kwa kuzingatia usalama, ikigusa makundi mengi, na kuhakikisha rasilimali hii inauzwa soko kuu na inanufaisha wote.
Ombi kwa Serikali
kikundi hiki, licha ya kutambuliwa rasmi, kinaomba kupatiwa leseni ya kuchimba iwasaidie kipato cha kuwawezesha kuendeleza ari ya kuwalinda wengine pamoja na vifaa zaidi vya kuwasaidia walindapo wengine.
Na hii ni sehemu ya hadithi kubwa ya madini – ni maisha, ni utajiri.
Madini ni Ajira, Uchumi na Maendeleo