WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa makundi mbalimbali ya kijamii kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii.
Amesema Serikali inafanya hivyo kwa kutambua kuwa kundi la Wajasiriamali ni muhimu na nguzo katika katika kukuza uchumi wa Taifa kupitia shughuli zao.
Amesema hayo leo Ijumaa (Oktoba 17, 2025) wakati wa mkutano wake na makundi mbalimbali ya Wajasiriamali wa jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla iliyofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini humo.
“Ninyi no watu muhimu sana kwenye uchumi wa nchi hii, na mmetoa mchango mkubwa sana kwenye uchumi wa nchi hii, nataka niwahakikishie Serikali hii inanufaika nawe na ndio maana Serikali inaendelea kuwathamini na inapanga mipango mbalimbali juu yenu, Endeleeni kuimarisha biashara zenu, hatutawatupa mkono”
Amesema kuwa katika kuhakikisha kundi hilo linanifaika, Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetekeleza programu mbalimbali zenye lengo la kuwawezesha Wajasiriamali nchini ikiwemo Utekelezaji wa programu zakuwezesha wananchi kupata mitaji, Masoko na mafunzo ya ujasiriamali
Programu nyingine ni Programu ya Taifa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi, kusimamia uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo kupitia programu za uwezeshaji wajasiriamali, Uendelezaji wa kongani za wajasiriamali pamoja na kutenga maeneo katika kila Halmashauri kwa ajili ya shughuli za kilimo, viwanda, biashara na shughuli nyingine muhimu za kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa Serikali itaendelea msukumo wa kuhamasisha na kusimamia uanzishwaji na usajili wa vikundi vyenye mwelekeo wa ushirika na makampuni, pamoja na kuwawezesha kupata mitaji na elimu ya matumizi ya mitaji hiyo ili waweze kuendesha shughuli zao kwa uhakika
“Viongozi kwenye halmashauri, fuatilieni mienendo ya biashara za Wajasiriamali katika maeneo yenu, ikiwa kuna changamoto zitatueni, lengo ni kuona kama tunapata ufanisi au la, lazima tujue wanafanikiwa kwa kiasi gani”
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali itaanzisha programu maalumu za kuwawezesha vijana waliomaliza taasisi za elimu ya juu na kati kuingia katika ajira na kujiajiri. “Programu hizi zitahakikisha vijana wanapata mitaji, elimu ya ujasiriamali, ardhi, na mazingira wezeshi ili kushiriki kikamilifu katika shughuli wanazokusudia”.
Naye, waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima amesema kuwa anamshukuru Rais Dkt. Samia kwa kusimamia maono yake ya kuhakikisha kuwa ananyanyua kundi la Wajasiriamali ili yaende safari ndefu ya kumiliki uchumi wa Tanzania
Wakizungumza katika mkutano huo, viongozi wa Wajasiriamali hao wameishukuru Serikali ya awamu ya Sita kwa jitihada mbalimbali ambazo imekuwa ikizifanya katika kuhakikisha kundi hilo linaendelea kustawi na kusaidia katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.