Featured Kitaifa

SEPESHA RUSHWA MARATHON 2025 YAZINDULIWA DODOMA

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu, Dodoma 

Mbio maarufu za Sepesha Rushwa Marathon msimu wa nne zimezinduliwa leo Oktoba 16, 2025 jijini Dodoma, zikiwa na lengo la kutoa elimu juu ya madhara ya rushwa na kuwaunganisha Watanzania kupitia michezo. Mbio hizo zinatarajiwa kufanyika Novemba 30, 2025 katika Uwanja wa Jamhuri.

Akizindua mbio hizo, Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Dodoma, Eugenius Bernard, amesema mbio hizo ni jukwaa muhimu la mapambano dhidi ya rushwa kwa ajili ya maendeleo ya kweli ya taifa.

“Kaulimbiu ya mwaka huu, Sepesha Rushwa Kimbia kwa Uadilifu (Run for Integrity) inabeba ujumbe mzito kwani lengo si tu kukimbia, bali kuunganisha nguvu ya pamoja na kufikisha ujumbe wa kupambana na rushwa kama jukumu la wote,”amesema. 

 

Amebainisha kuwa TAKUKURU Dodoma haisimami kama mlinzi wa sheria pekee, bali kama mshirika wa wananchi katika kulinda rasilimali za umma, haki na utu wa kila Mtanzania, huku akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na wananchi ni nguzo muhimu ya mafanikio.

 

“Taasisi hii imekuwa mhamasishaji mkubwa kupitia kampeni ya Badili Tabia, Sepesha Rushwa, ambayo imeleta uelewa kwa vijana, wanawake, viongozi wa dini, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla,” amesema.

Aidha, amesema utekelezaji wa kampeni hiyo umeongeza uelewa na utayari wa wananchi kuripoti vitendo vya rushwa, tofauti na ilivyokuwa awali.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Sauti ya Wapinga Rushwa, Eliasa Abdallah, amesema wanatarajia washiriki zaidi ya 2,500 katika mbio hizo.

“Sepesha Rushwa Marathon inalenga mambo matatu makuu Kutoa elimu ya rushwa kwa wananchi, Kuadhimisha Siku ya Kupinga Rushwa Duniani Desemba 9 na Kukusanya fedha za kuendesha kampeni ya Badili Tabia – Sepesha Rushwa,”amesema. 

Kwa mujibu wa Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa mwaka 2023/24  zilizowasilishwa Machi 27, 2025, zilionyesha mafanikio katika baadhi ya sekta, lakini pia zilibaini changamoto kadhaa, zikiwemo kasoro katika usimamizi wa fedha za umma.

 

 

 

 

About the author

mzalendo