Featured Kitaifa

MAKAMU WA RAIS AZINDUA JENGO LA HIFADHI YA URITHI WA KIJIOLOJIA LA NGORONGORO

Written by Alex Sonna

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian akizindua Jengo la Makumbusho ya Eneo la Hifadhi ya Urithi wa Kijiolojia la Ngorongoro – Lengai lililopo Karatu mkoani Arusha leo tarehe 16 Oktoba 2025.

…..

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema suala la utunzaji wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi linapaswa kupewa kipaumbele katika uendelezaji na ukuzaji utalii ili kuepukana na kuvurugika kwa ikolojia na hatari dhidi ya ustawi wa shughuli za utalii. 

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akizindua Jengo la Makumbusho ya Eneo la Hifadhi ya Urithi wa Kijiolojia la Ngorongoro – Lengai lililopo Karatu mkoani Arusha. Amesema kutokana na uharibifu wa mazingira, inashuhudiwa muingiliano kati ya wanyamapori na binadamu unaopelekea athari kubwa zaidi, vikiwemo vifo na uharibifu wa makazi na mazao.

Aidha, Makamu wa Rais ametoa rai kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, kupitia Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuhakikisha miundombinu ya makumbusho hayo inatunzwa na kutumika kama ilivyokusudiwa. Vilevile, amesema ni muhimu kuweka utaratibu mzuri utakaowezesha ukarabati na matengenezo ya mara kwa mara ya miundombinu na mifumo iliyowekwa katika jengo hilo.

Halikadhalika , Makamu wa Rais ameitaka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kufanya jitihada za makusudi kushirikisha jamii inayozunguka eneo hilo katika shughuli za uhifadhi wa eneo hilo, zikiwemo mila na tamaduni zake. Pia ametoa wito kwa Watanzania, kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio na maeneo ya kihistoria ili kujifunza na kujionea utajiri mkubwa ambao nchi imejaaliwa. 

Makamu wa Rais amesema ni vema Wizara kwa kushirikiana na Taasisi zake ikiwemo Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, ihakikishe inatoa mafunzo stahiki kwa watumishi watakaohudumu katika eneo hilo ili kuwawezesha watumishi hao kutumia mifumo iliyopo na kutoa huduma kwa ufasaha na ufanisi. Amesema kwa kadri itakavyowezekana, mafunzo hayo yashirikishe wadau wa utalii ambao  wana mchango katika kuleta wageni watakaokuja kujifunza kupitia utalii wa mambo mbalimbali yaliyopo katika kituo hicho.

Makamu wa Rais amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali za makusudi ili kuhakikisha inaboresha huduma za utalii, ikiwemo kutengeneza filamu mbili maarufu za “Tanzania: The Royal Tour” na “Amazing Tanzania” . Hatua nyingine zilizochukuliwa ni pamoja na kuboresha miundombinu mbalimbali ya utalii hususan barabara, hoteli, nyumba za kulala wageni, viwanja vya ndege na nyinginezo. Pia, kurahisisha upatikanaji wa visa, kuimarisha usalama wa watalii, kuwekeza katika maendeleo ya rasilimaliwatu na kuimarisha taswira ya Tanzania duniani. 

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana amesema mageuzi makubwa yaliyofanyika katika Wizara hiyo yamepelekea kuimarika kwa sekta ya utalii kwa kuongeza watalii wa kimataifa kutoka watalii milioni 1.8 mwaka 2023 hadi kufikia watalii milioni 2.1 mwaka 2024. Pia amesema idadi ya watalii wa ndani kuongezeka kutoka milioni 1.9 hadi milioni 3.2. 

Halikadhalika ametaja mafanikio mengine ni pamoja na kuimarika kwa ulinzi na usimamizi wa wanyamapori kupitia mkakati madhubuti wa kudhibiti ujangili, kuimarisha doria na matumizi ya teknolojia. Amesema idadi ya wanyamapori inazidi kuongezeka pamoja na hali ya usalama katika maeneo ya hifadhi. 

Mradi wa Jengo la Makumbusho ya Eneo la Hifadhi ya Urithi wa Kijiolojia la Ngorongoro – Lengai umegharimu shilingi bilioni 32 na kufadhiliwa na Serikali ya China.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Viongozi mbalimbali wakati alipowasili Karatu mkoani Arusha kuzindua Jengo la Makumbusho ya Eneo la Hifadhi ya Urithi wa Kijiolojia la Ngorongoro – Lengai leo tarehe 16 Oktoba 2025.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akitembelea Jengo la Makumbusho ya Eneo la Hifadhi ya Urithi wa Kijiolojia la Ngorongoro – Lengai kabla ya kuzindua jengo hilo lililopo Karatu mkoani Arusha leo tarehe 16 Oktoba 2025.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikabidhiwa mfano wa funguo kutoka kwa Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian kuashiria kukabidhi Jengo la Makumbusho ya Eneo la Hifadhi ya Urithi wa Kijiolojia la Ngorongoro – Lengai lililofadhiliwa na Serikali ya China, wakati wa uzinduzi wa jengo hilo uliyofanyika Karatu mkoani Arusha leo tarehe 16 Oktoba 2025.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian akizindua Jengo la Makumbusho ya Eneo la Hifadhi ya Urithi wa Kijiolojia la Ngorongoro – Lengai lililopo Karatu mkoani Arusha leo tarehe 16 Oktoba 2025.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian katika picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania na China mara baada ya kuzindua Jengo la Makumbusho ya Eneo la Hifadhi ya Urithi wa Kijiolojia la Ngorongoro – Lengai lililopo Karatu mkoani Arusha leo tarehe 16 Oktoba 2025.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akishuhudia utiaji Saini wa makabidhiano wa Jengo la Makumbusho ya Eneo la Hifadhi ya Urithi wa Kijiolojia la Ngorongoro – Lengai wakati wa hafla iliyofanyika Karatu mkoani Arusha leo tarehe 16 Oktoba 2025.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia mara baada ya kuzindua Jengo la Makumbusho ya Eneo la Hifadhi ya Urithi wa Kijiolojia la Ngorongoro – Lengai lililopo Karatu mkoani Arusha leo tarehe 16 Oktoba 2025.

default

Picha za Jengo la Makumbusho ya Eneo la Hifadhi ya Urithi wa Kijiolojia la Ngorongoro – Lengai lililozinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango lililopo Karatu mkoani Arusha leo tarehe 16 Oktoba 2025.

About the author

Alex Sonna