Featured Kitaifa

BENKI YA DUNIA KUSAIDIA TANZANIA KUWEKEZA KWENYE NISHATI NA SGR

Written by Alex Sonna

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (kushoto) akiagana na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiamé Diop, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo makao makuu ya Benki hiyo jjini Washington D.C, nchini Marekani, ambapo kunafanyika pia Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, pamoja na mambo mengine walijadiliana kwa kina benki hiyo kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa nishati ya umeme itakayotumiwa na nchi za Afrika ili kulinda usalama wa kiuchumi na uzalishaji wa bidhaa katika kipindi kifupi kijacho pamoja na kuongeza thamani ya mradi wa treni iendayo kasi (SGR) ili iweze kuwanufaisha wananchi na wawawekezaji katika korido ambayo miundombinu ya treni itapita.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, akizungumza jambo wakati wa kikao cha ujumbe wa Tanzania na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiamé Diop (hayupo pichani), uliofanyika makao makuu ya benki hiyo jijini Washington D.C, nchini Marekani, ambapo
aliishukuru Benki hiyo kwa kuiwezesha Tanzania kutekeleza miradi mingi ya kimkakati inayochochea ukuaji wa uchumi wa nchi na maendeleo ya wananchi kwa ujumla.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (wa tatu kushoto) na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiamé Diop (Katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe kutoka Tanzania na Benki ya Dunia, Katibu Mkuu-Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil (wa tatu kulia) Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Dkt. Elsie Kanza (wa pili kushoto), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban (wa pili kulia), Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, anayeziwakilisha pia nchi za Malawi, Zambia na Zimbabwe, Bw. Nathan Belete (wa kwanza kushoto) ,baada ya kukutana na kufanya mazungumzo makao makuu ya benki hiyo jijini Washington D.C, nchini Marekani.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Washington D.C, nchini Marekani)

Na Benny Mwaipaja, Washington D.C, Marekani

BENKI ya Dunia imeahidi kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa nishati ya umeme itakayotumiwa na nchi za Afrika ili kulinda usalama wa kiuchumi na uzalishaji wa bidhaa katika kipindi kifupi kijacho pamoja na kuongeza thamani ya mradi wa treni iendayo kasi (SGR) ili iweze kuwanufaisha wananchi na wawawekezaji katika korido ambayo miundombinu ya treni itapita.

Ahadi hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiamé Diop, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania, unaoongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, kwenye Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, inayofanyika Jijini Washington D.C, nchini Marekani.

Dkt Diop alisema kuwa Tanzania ni nchi iliyojaaliwa kuwa na vyanzo muhimu vya kuzalisha nishati na kwamba uzalishaji wa nishati utakaofanyika utakuwa na manufaa kwa uchumi wa Tanzania kwa kufanya biashara ya kuuza umeme kwenye nchi nyingine.

“Tungependa kusaidia mradi huu wa kuzalisha umeme katika ikipindi kifupi, ikiwezekana katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa ili Tanzania na Afrika iwe na umeme wa uhakika utakaokuza uwekezaji na uzalishaji.” Alisema Dkt. Diop

Kuhusu ujenzi wa miundombinu ya SGR, Dkt. Diop alibainisha kuwa Benki ya Dunia iko tayari kusaidia reli hiyo kwa kutoa fedha zitakazo jenga miundombinu itakayo changia kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi kwa wananchi katika maeneo ambayo reli hiyo inapita.

Aidha, alipongeza uhusiano imara uliopo kati ya Tanzania na Benki ya Dunia na kuahidi kuwa Benki yake itaendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada zake za kukuza uchumi na kuwaondolea umasikini wananchi wake kwa kusaidia fedha zitakazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii pamoja na kutoa misaada ya kiufundi itakayochochea ukuaji wa uchumi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, aliishukuru Benki hiyo kwa kuiwezesha Tanzania kutekeleza miradi mingi ya kimkakati inayochochea ukuaji wa uchumi wa nchi na maendeleo ya wananchi kwa ujumla.

Alisema kuwa ahadi iliyotolewa na Benki ya Dunia katika kusaidia utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo SGR, nishati, kilimo, afya, elimu na ujenzi wa miundombinu, italeta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania na katika ukanda wa Afrika kwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa shughuli za uzalishaji mali na kukuza ajira kwa wananchi hususan vijana.

Uwekezaji wa Benki ya Dunia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania umefikia dola za Marekani bilioni 10.9 ambapo miradi 38 ya maendeleo inatekelezwa katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, maji, elimu, nishati, ujenzi wa miundombinu ya Barabara, ujenzi wa masoko na miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

About the author

Alex Sonna