Featured Kitaifa

SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA HUDUMA ZA USTAWI KWA WAZEE.

Written by Alex Sonna

Na Jackline Minja – WMJJWM
Dar Es Salaam.

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kudumisha huduma bora kwa wazee kwa kuhakikisha kundi hilo linapata huduma za msingi zinazowawezesha kuishi maisha yenye heshima na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu tarehe 15 Oktoba, 2025 wakati wa ziara yake katika Makazi ya Wazee Wasiojiweza cha Tushikamane Pamoja Foundation yaliyopo Kata ya Kwembe, Manispaa ya Ubungo mkoani Dar Es Salaam.

Dkt. Jingu amesema wazee ni sehemu ya taifa kwakua wamelitumikia kwa muda mrefu kwa uaminifu na kujitolea hivyo jamii ya Watanzania wana wanawajibu wa kuwasaidia na kuwaenzi wazee kama ishara ya kuthamini mchango wao kwa maendeleo ya nchi.

“Lengo la kuwatembelea ni kuwaona kuwajulia hali na kuendelea kuwaenzi pamoja na kuthamini mchango wenu mkubwa katika kujenga na kuimarisha jamii yetu ya Tanzania, ninatambua kazi nzuri inayofanywa hapa katika kutoa huduma bora, upendo na matunzo kwa Wazee wetu.” amesema Dkt. Jingu

Aidha amewapongeza wamiliki na waendeshaji wa makazi hayo kwa moyo wa kujitolea wanaouonesha vilevile amewapongeza Manispaa ya Ubungo kwa usimamizi na uratibu wa Makazi hayo jambo linaloonesha dhamira njema ya kuhakikisha wazee wanaishi katika mazingira salama.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti Msaidizi wa Makazi ya Wazee Tushikamane Pamoja Foundation Sada Jaha amesema changamoto kubwa katika Makazi hayo ni uhaba wa watumishi ambao wanawahudumia wazee hao na amewaomba wadau na Mashirika mbalimbali kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwaenzi na kuwatunza wazee hao.

“Tunamshukuru sana Katibu Mkuu kwa kuja kutusikiliza na kutuahidi na kutuhakikishia kuwa changamoto tulizonazo zitapatiwa ufumbuzi kwa kuwa Serikali hii ni sikivu na inawajali na kuwapa kipaumbele suala la ustawi kwa wazee.” amesisitiza Sada

Nao baadhi ya Wazee waliopo katika Makazi hayo wameishukuru Serikali kwa kuwakumbuka na kuwatembelea kambini hapo ambapo kitendo hicho kinazidi kuwapa faraja na matumaini ya kuendelea kuishi na kujiona na umuhimu kama watu wengine.

About the author

Alex Sonna