Mbele ya maelfu ya wanachama wa Chama chake na wananchi wa Missenyi leo Jumatano Oktoba 15, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kyaka, Dkt. Samia amesema kuwa uwanja huo mkubwa na wa kisasa unatarajiwa kufungua fursa mpya za uwekezaji na kukuza sekta ya utalii, biashara na kilimo biashara ndani ya mkoa wa Kagera na maeneo jirani.
“Tumeanza kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya kujenga uwanja mkubwa na wa kisasa katika eneo la Kyabajwa. Awali, ilipendekezwa Omukajunguti, lakini eneo hilo halikufaulu vizuri katika upembuzi yakinifu, hivyo tumeamua kujenga Kyabajwa.” Amesema Dkt. Samia.
Kulingana na Dkt. Samia, uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege kubwa za kimataifa kama Boeing 737-900, zenye uwezo wa kubeba abiria 180 hadi 220, jambo litakalofungua milango ya kiuchumi na fursa za biashara kwa wananchi wa Missenyi na maeneo ya mpakani mwa Tanzania na Uganda.
Ameongeza kuwa mradi huo ni sehemu ya juhudi za serikali za kuimarisha miundombinu ya usafiri na kusukuma mbele sera ya kilimo biashara, kwa kuwezesha usafirishaji wa mazao na bidhaa za kibiashara kwenda ndani na nje ya nchi.