Featured Kitaifa

WADAU WAONYA VIJANA KUEPUKA VURUGU KIPINDI CHA UCHAGUZI

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Katika kipindi ambacho joto la kisiasa linazidi kupanda na mitandao ya kijamii ikiwaka kwa mijadala mikali, Wadau mbalimbali wameanza kuibuka na kukemea vikali vijana kuepuka kushawishiwa kushiriki maandamano yasiyo halali, vurugu na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani ya nchi.

Onyo hilo linakuja baada ya kugundulika kwamba baadhi ya makundi yanaanza kujaribu kutumia hamasa za vijana kama “silaha ya kisiasa”, badala ya kuwapa elimu ya kupiga kura kwa amani.

Akizungumza Jiji Dodoma Mwanasheria wa Machifu Tanzania Samwel Chimanyi amesema Vijana si jeshi la mitaani, bali ndiyo nguvu ya maendeleo, hivyo wasikubali kutumika katika kuvuruga amani ya nchi.

“Tangu mwaka 1992 tulipoanza mfumo wa vyama vingi tukaanza kupiga kura 1995, ikifika kipindi cha uchaguzi yanaibukaga makundi changanyikeni tunaita, yakishaibuka makundi mengine yanakuja kwaajili ya utafutaji yaani “Wasaka Tonge”, kwahiyo hawa wasakatonge ndiyo huwa wanaleta vurugu hizo kwamba wanatumia fursa ya watanzania walio wanyonge ambao wana uelewa mdogo kwenda kudanganya,”amesema.

Aidha, amewakumbusha watanzania kurudi nyuma na kuangalia historia ya nchi ilipotoka katika mikono ya wakoloni ambapo baada ya hapo imekuwa huru ila kwasasa zimezuka propaganda ambazo ni mbaya kwa taifa licha ya kazi kubwa iliyofanywa na viongozi waliopita.

“Leo hii wanazuka watu wanakuja na pesa wanalipa watu, sasa nakumbusha kwamba tujiangalie sana na kundi linalotumiwa sana ni kundi la vijana kwamba mkalete Vaibu, tusilete vaibu tutunze heshima zetu, wewe ni kijana lakini utakuwa na familia hivyo tusiingie kwenye makundi yasiyofaa,”amesema.

Chimanyi ameongeza kuwa, kwasasa kuna watu wametengeneza mfumo feki wa kupotosha ambao ni hatari kwa taifa unaitwa “rambaramba” ambapo ukiwaramba watanzania fahamu zao kwenye uchaguzi hawawezi kwenda kupiga kura.

“Mpaka sasa tulipofikia hapa watanzania kila mmoja ajue kabisa kama alikuwa ajui Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imefanya kazi kubwa, imefanya kazi kwa weledi kwa umakini wa hali ya juu kuratibu na kusimamia zoezi zima la mchakato wa uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani huu mwaka na Tume hii imekuwa mfano wa kuigwa hata kwa mataifa mengine kutoka na kazi nzuri wanayoifanya kuja kujifunza kwao,”ameongeza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa taasisi ya wafikiliaji duniani (TAWADU), Chifu William Machimu amesema nchi ipo salama lakini wanapaswa kufikilia upya namna bora ya kusimamia usalama uliopo.

“Niombe ujumbe huu uwafikie watanzania wote kuwa hatuitaji machafuko, vurugu na vita kwasababu ya jambo la uchaguzi, jambo la uchaguzi ni jambo lililowahi kufanyika miaka mingine tangu kuanzishwa kwa uhuru, kwahiyo tunaenda kwenye uchaguzi tukiwa tunajua ni desturi yetu kila baada ya miaka mitano, “amesema.

Naye Mwenyekiti wa wanawake na Samia mkoa wa Dodoma Bi. Fatma Madidi amewaomba wale walioanzisha magenge mbalimbali wayavunje na wanao hamasishana mitandaoni kuacha kwani amani inahitajika nchini.

“Niwaombe watanzania wote tuitunze amani hii tuliyonayo, kila mmoja ageuke awe mwelimishaji na mhamasishaji kwa mwenzake kuhakikisha kuwa taifa linakuwa na amani na tunavuka salama katika kipindi hiki cha joto la uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025,”amesema.

Mwisho.

About the author

mzalendo