Featured Kitaifa

MAJALIWA AIPONGEZA VETA KWA KUWAWEZESHA VIJANA WENYE ULEMAVU KUJIAJIRI

Written by Alex Sonna

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameipongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa jitihada zake za kuwawezesha vijana wenye mahitaji maalum kupata ujuzi wa kazi, akisema hatua hiyo ni mfano halisi wa utekelezaji wa dhana ya ushirikishwaji kwa vitendo.

Majaliwa alitoa pongezi hizo jana tarehe 10 Oktoba, 2025 alipokuwa akitembelea banda la VETA katika maadhimisho ya Wiki ya Vijana yanayofanyika mkoani Mbeya, ambako alishuhudia vijana wenye ulemavu wakiwasilisha kazi zao katika fani mbalimbali ikiwemo ushonaji wa nguo na teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).

Katika banda hilo, Waziri Mkuu alikutana na Francis Anthony, mhitimu wa VETA ambaye kwa sasa ni mwalimu wa kompyuta. Francis alieleza jinsi alivyopata mafunzo na baadaye kuajiriwa kufundisha vijana wengine.

“Nilianza kama mwanafunzi wa VETA, sasa ninafundisha. Hii ni ishara kuwa vijana wenye ulemavu wakipewa nafasi, wana uwezo wa kuchangia maendeleo ya taifa,” alisema Francis.

Kwa upande wake, Mwanafunzi wa VETA Songea,Riziki Ndumba, alisimulia jinsi alivyoweza kumaliza kozi ya ushonaji licha ya kuanza mafunzo bila kuwa na ujuzi wowote.

“Kwa msaada wa walimu na mazingira rafiki, nimeweza kujifunza na sasa ninaweza kujitegemea,” alisema Riziki.

Akizungumzia mipango ya taasisi hiyo, Ofisa Uhusiano wa VETA, Eimer Sarao, alisema mamlaka imejipanga kuhakikisha vijana wenye ulemavu wanapata fursa sawa za mafunzo ya ufundi ili kuondoa vikwazo vinavyosababisha utegemezi.

“Tuna walimu waliowahi kuwa wanafunzi wetu wenye ulemavu. Mfano mzuri ni mwalimu anayefundisha katika Chuo cha Mafunzo Stadi Morogoro. Hii inaonyesha kuwa ulemavu si kikwazo cha mafanikio,” alisema Sarao.

VETA inaendelea kutekeleza programu maalum zinazolenga makundi mbalimbali ya kijamii, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kujenga taifa lenye nguvu kazi jumuishi, lenye stadi na tija kwa uchumi wa sasa na ujao.

About the author

Alex Sonna