MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari,akizungumza leo Oktoba 7, 2025, jijini Dodoma, wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa mawakili wa serikali kuhusu masuala ya ubia, yaliyoandaliwa na Kituo cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC).
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari,akizungumza leo Oktoba 7, 2025, jijini Dodoma, wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa mawakili wa serikali kuhusu masuala ya ubia, yaliyoandaliwa na Kituo cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC).
MKURUGENZI wa Huduma za Sheria kutoka PPPC, Bi. Flora Tenga,akizungumza wakati wa mafunzo ya siku tatu kwa mawakili wa serikali kuhusu masuala ya ubia, yaliyoandaliwa na Kituo cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC).
MKURUGENZI wa Huduma za Sheria kutoka PPPC, Bi. Flora Tenga,akizungumza wakati wa mafunzo ya siku tatu kwa mawakili wa serikali kuhusu masuala ya ubia, yaliyoandaliwa na Kituo cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC).
SEHEMU ya washiriki wakimsikiliza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari (hayupo pichani),wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa mawakili wa serikali kuhusu masuala ya ubia, yaliyoandaliwa na Kituo cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC).
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua mafunzo ya siku tatu kwa mawakili wa serikali kuhusu masuala ya ubia, yaliyoandaliwa na Kituo cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC).
Na Alex Sonna-DODOMA
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari, amewataka mawakili wa serikali kuhakikisha maslahi ya taifa yanapewa kipaumbele wakati wa majadiliano na usimamizi wa mikataba ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP), ili miradi hiyo iwe na manufaa kwa Watanzania.
Mhe. Johari ametoa wito huo leo Oktoba 7, 2025, jijini Dodoma, wakati wa kufungua mafunzo ya siku tatu kwa mawakili wa serikali kuhusu masuala ya ubia, yaliyoandaliwa na Kituo cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC).
Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha mawakili wa Serikali kuelewa kwa kina dhana ya PPP, sheria na mwongozo wake, pamoja na namna bora ya kusimamia, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa miradi ya ubia kati ya Serikali na sekta binafsi.
Amesema kuwa mafunzo hayo yanatarajiwa kuwajengea uwezo mawakili wa serikali kuhusu misingi ya miradi ya ubia, mfumo wa kisheria unaosimamia PPPC nchini, usimamizi wa vihatarishi, majadiliano na usimamizi wa mikataba ya ubia, pamoja na mifumo ya kifedha inayotumika katika utekelezaji wa miradi hiyo.
“Naamini baada ya mafunzo haya, mawakili wa serikali wataimarika katika kushauri, kujadiliana na kusimamia masuala ya kisheria kuhusu mikataba ya PPPC kwa ufanisi, huku wakihakikisha maslahi ya taifa yanabaki kuwa kipaumbele,” amesema Mhe.Johari
Aidha ameongeza kuwa mikataba ya ubia ni nyenzo muhimu katika kufanikisha maendeleo ya taifa, hivyo ni lazima iandaliwe kwa umakini na kwa kuzingatia maslahi ya muda mrefu ya nchi.
“Hii itasaidia kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ikiwemo kuboresha maisha na kuongeza kipato kwa wananchi,” amesisitiza Mhe. Johari.
Hata hivyo amesema kuwa serikali imeweka misingi madhubuti ya kisheria na kitaasisi kusimamia miradi ya ubia, ikiwa ni pamoja na kutungwa kwa sera na sheria husika, ili kuhakikisha ubia huo unaleta manufaa kwa pande zote mbili.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka PPPC, Bi. Flora Tenga, amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo mawakili wa serikali ili waweze kusimamia mikataba ya ubia kwa ufanisi na kuliepusha taifa na hasara.
“Mwanasheria Mkuu ndiye mwenye jukumu la kutekeleza mikataba ya ubia kwa niaba ya serikali. Hivyo ni muhimu mawakili wake wakapata mafunzo haya ili kuepuka makosa ya kisheria yanayoweza kulisababishia taifa hasara,” amesema Bi. Tenga.
Aidha ameongeza kuwa mikataba yoyote lazima ipitie hatua stahiki, ikiwemo tathmini ya thamani ya fedha, maandiko ya kisheria na ukaguzi wa kina kabla ya kutiwa saini. Kukosekana kwa mojawapo ya hatua hizo kunaweza kuleta changamoto kubwa.
Naye Mshiriki Moja kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw.Stanslaus Silayo,ametoa shukrani kwa Kituo cha PPPC kuwapa mafunzo hayo ambayo yatawasaidia kuingia mikataba yenye tija kati ya serikali na sekta binafsi na kupunguza hatari ya hasara kwenye miradi ya ubia.