Featured Kitaifa

SERIKALI YARIDHISHWA NA MRADI WA UMEME WA JUA SHINYANGA

Written by Alex Sonna
Msimamizi wa mradi wa uzalishaji umeme unaotokana na jua katika Kijiji cha Ngunga, Kata ya Talaga, Wilayani Kishapu, Mkoani Shinyanga Emmanuel Mbando akitoa ufafanuzi

 

Mhandisi wa Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Innocent Luoga (kushoto) akitembelea mradi mradi wa uzalishaji umeme unaotokana na jua katika Kijiji cha Ngunga, Kata ya Talaga, Wilayani Kishapu, Mkoani Shinyanga

 

Na Mwandishi wetu – Malunde 1 blog
 
Serikali imeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa uzalishaji umeme unaotokana na jua katika Kijiji cha Ngunga, Kata ya Talaga, Wilayani Kishapu, Mkoani Shinyanga, baada ya kufikia asilimia 78 ya utekelezaji wa awamu ya kwanza.
 
Mradi huu utazalisha Megawati 50 ambazo zitaingizwa kwenye gridi ya taifa, kuongeza usambazaji wa umeme kwa wananchi.
 
Akizungumza Oktoba 06, 2025, Mhandisi wa Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Innocent Luoga, amesema ziara hiyo ililenga kutembelea mradi huo ili kukagua maendeleo yake na kuona jinsi unavyoweza kupunguza gharama za umeme kwa wananchi.
“Katika Awamu ya kwanza ya mradi huu utazalisha Megawati 50 ambazo zitaingizwa kwenye gridi ya taifa, kwa lengo la kusambaza umeme kwa wananchi na kuleta unafuu,” amesema Mhandisi Luoga.
 
Aidha, amesisitiza kuwa mradi utaendelea kufanyika kulingana na mkataba uliopo.
 
“Tunataka tuwe na vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme, tusitegemee vyanzo vichache. Kwa sasa tunategemea maji na gesi, lakini sasa tunaanza kutumia vyanzo mbadala kama umeme wa jua, upepo, na joto la ardhi”,ameeleza Mhandisi Luoga.
 
Amefafanua kuwa kuongezwa kwa vyanzo hivi kunachangia usalama wa nishati nchini, kwani hata pale maji au gesi itakapokosekana, wananchi wataendelea kupata huduma za umeme.
Mhandisi Luoga pia ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluu Hassan kwa kuweka fedha nyingi katika sekta ya nishati, jambo lililosaidia kufanikisha mradi huo.
“Kwa Mkoa wa Shinyanga, mahitaji ya umeme ni Megawati 102, lakini zipo zaidi, na uwepo wa kituo hiki unatarajiwa kuongeza megawati zaidi”,amesema.
 
Msimamizi wa mradi, Emmanuel Mbando, amesema utekelezaji ulianza Desemba 8, 2023, na wanatarajia awamu ya kwanza ya Megawati 50 kukamilika ifikapo Desemba mwaka huu ili kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
 
Ameongeza kuwa mradi unatekelezwa kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza ni Megawati 50, kisha utekelezaji wa Megawati 100 kufikia jumla ya 150.
 
Mradi mzima unatarajia kugharimu shilingi bilioni 323 kwa awamu zote mbili.
Mhandisi wa Umeme na Nishati Jadidifu, Innocent Luoga, akizungumza na viongozi mbalimbali baada ya kutembelea mradi wa kuzalisha umeme wa jua, hatua muhimu katika kuongeza usambazaji wa umeme na kuimarisha usalama wa nishati nchini.
Msimamizi wa mradi wa uzalishaji umeme unaotokana na jua katika Kijiji cha Ngunga, Kata ya Talaga, Wilayani Kishapu, Mkoani Shinyanga Emmanuel Mbando akitoa ufafanuzi
Mhandisi wa umeme na Nishati jadidifu kutoka Wizara ya Nishati Innocent Luoga mkono wa kushoto akizungumza na msimamizi wa Mradi huo Emmanuel Mbando
Alhaji Mhandisi Abdala Fereshi akitoa ufafanuzi namna ambavyo mradi unatekelezwa
Msimamizi wa mradi wa uzalishaji umeme unaotokana na jua katika Kijiji cha Ngunga, Kata ya Talaga, Wilayani Kishapu, Mkoani Shinyanga Emmanuel Mbando akitoa ufafanuzi
Ukaguzi wa mradi unaendelea
Ujenzi unaendelea
Ujenzi unaendelea
Baadhi ya majengo yanayoendelea kujengwa kwenye mradi wa uzalishaji umeme wa jua

About the author

Alex Sonna