Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Ndugu Kenani Kihongosi,akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 5, 2025) katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi Kuu ya CCM jijini Dodoma
Na.Alex Sonna-DODOMA
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Ndugu Kenani Kihongosi, amesema kuwa tangu kuanza kwa kampeni za Urais kupitia CCM kwa mgombea wake Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, zaidi ya wananchi milioni 45 tayari wameshiriki kwa namna mbalimbali.
Hata hivyo Kihongosi,ameongeza kuwa kampeni hizo zimekuwa za kistaarabu na hazijajikita katika siasa za matusi au kejeli, bali zimebeba ujumbe wa matumaini, mshikamano, na maendeleo jumuishi ya taifa.
Aidha, ameeleza kuwa kuanzia Oktoba 7, 2025, mgombea huyo ataendelea na ziara zake katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, ikiwemo Simiyu, Mwanza na Mara, ambapo atazungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara, kuwasilisha sera na kuelezea kwa kina dhamira ya CCM ya kuijenga Tanzania ya kisasa na yenye ustawi wa kiuchumi.
“Tunawaomba wananchi waendelee kujitokeza kwa wingi katika mikutano hiyo, wakimsikiliza mgombea wetu ambaye amejidhihirisha kuwa ni kiongozi mwenye dira, busara na uwezo wa kuyaongoza mageuzi ya kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya wote,” alisisitiza.
Amehitimisha kwa kusema kuwa CCM itaendelea kuendesha kampeni zake kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, huku ikihimiza amani na mshikamano kwa kila hatua ya mchakato wa uchaguzi.