Rufiji, Pwani
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Luteni Kanali Fredrick Komba ameipongeza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kurejesha mawasiliano ya miundombinu ya barabara katika wilaya yake.
Amesema wilaya ya Rufiji kwa mwaka 2023/2024 ilipata mafuriko ambayo yaliathiri şana miundombinu ya barabara katika tarafa ya Mohoro, Ikwiriri pamoja na Mkongo.
“TARURA imeweza kufanya kazi nzuri kwa nafasi yake kwani kwa muda mfupi imeweza Kurekebisha hitilafu zilizotokana na mafuriko“.
Akitolea mfano Luteni Kanali Komba amesema TARURA imejenga barabara mpya za lami, ujenzi wa daraja la Mohoro lenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 17 ambalo linaunganisha vijiji viwili vya Ndundutawa na King’ongo zinazounganisha Makao Makuu ya Tarafa ya Mohoro na kijiji cha Kipoka katika Kata ya Chumbi.
“Naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutekeleza miradi mingi ya TARURA kwenye wilaya ya Rufiji“.
“Mimi na wananchi tunaweza kusafiri mahali popote kwenye wilaya hii, ujenzi wa miundombinu umeleta matumaini makubwa kwa wananchi wa Rufiji”, ameongeza.
Amesema Serikali imeonesha dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi kwa kuhakikisha miundombinu ya barabara inakua thabiti na wananchi kuweza kusafirisha mazao yao.
Kwa upande wake, Meneja wa TARURA wilaya ya Rufiji, Mhandisi Nicolaus Ludigery amesema kwamba miradi yote inayotekelezwa katika wilaya ya Rufiji inaenda kuwarahisishia wananchi shughuli za kijamii na kiuchumi.
Amesema barabara nyingi zilipata athari kubwa kutokana na mafuriko na kimbunga Hidaya, hivyo wamejipanga kuhakikisha miradi yote inakamilika kama ilivyokusudiwa.
Naye, Bi. Saida Mwilu mkazi wa Ikwiriri amesema ujenzi wa barabara za lami kwenye mji wa Ikwiriri zimewaletea manufaa makubwa hususan kwa wajasiriamali ambao hutembeza bidhaa zao mitaani kwani awali kipindi cha mvua kulikuwa na madimbwi ya maji na kuongeza kwamba taa za barabarani zitakapowekwa itawasaidia kufanya biashara hadi usiku na kwa usalama.
Pia, Bw. Malik Kitala mwendesha bodaboda ameishukuru Serikali kwa kuwatengenezea barabara kwani awali kutokana na ubovu wa barabara hasa kipindi cha mvua nauli zilikuwa juu.