Ikwiriiri, Rufiji
WAKALA ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoani Pwani, wapo katika hatua za kusitisha mikataba ya Makandarasi wawili wa kampuni ya HariCom International Ltd na Trinity Manufacturing Services kwa kushindwa kutekeleza ujenzi wa miradi ya miundombinu ya barabara kwa wakati.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila, wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi ya ukaguzi wa utekelezaji wa barabara inayofanyika Rufiji mkoani Pwani.
Amesema usitishwaji wa mikataba kwa Makandarasi hao inatokana na kushinda zabuni pamoja na kupewa malipo ya awali lakini wameshindwa kutekeleza mikataba yao.
“Kampuni ya HariCom International Ltd ilipata zabuni ya ujenzi wa barabara ya Polisi-Kirungi yenye urefu wa Km 1, ambapo walitanguliziwa kiasi cha shilingi milioni 160 lakini mpaka sasa hawajatengeneza barabara na kutelekeza vifaa vyao katika eneo la mradi,” amesema.
Ameongeza kuwa kampuni hiyo, mpaka kukamilika kwa mradi huo, gharama zake ingekuwa shilingi bilioni 1 na milioni 70.
Kwa upande wa kampuni ya TRINITY kampuni hiyo ilipatiwa malipo ya awali ya shilingi milioni 460 toka mwaka jana mwezi Agosti na mradi ulitakiwa uwe umekamilika mwaka huu, mwezi Novemba, lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea katika mradi huo.
Amesema Tanzania inapenda Makandarasi wazawa washiriki katika masuala ya ukandarasi, lakini baadhi ya wazawa wamekuwa sio waaminifu na kuchukuwa pesa na kushindwa kutekeleza miradi kwa wakati na kutimiza mikataba kama zabuni zilivyotangazwa.
Amesema hakuna ambaye hakusikia au kuona jinsi mvua za mwaka 2023 na 2024 jinsi zilivyoharibu mazingira ya makazi ya watu wa Rufiji, kutokana na kuharibika kwa makazi ya watu wa Rufiji kwa kuzingirwa na maji, ikiwamo kuharibika kwa mashamba suluhisho la kuwanusuru wanarufiji ni kuboresha miundombinu, ambayo itasaidia panapotokea mvua kunyesha changamoto tena zisitokee kwa jamii.
“Inasikitisha kampuni zinamajina makubwa kuchukuwa tenda na ‘advance’ lakini kutekeleza majukumu yao wameshindwa,” amesema.
Mhandisi Mativila amesema hatua zitachukuliwa kwa hayo makampuni yaliyoshindwa kufanya kazi kwa wakati ikiwamo kushikilia vitu vyao ambavyo walivitanguliza katika maeneo ya mradi.
Ameongeza kuwa kutokana na kushindwa kutekeleza miradi hiyo, ameomba Makandarasi hao wasipewe kazi zozote kupitia TAMISEMI.
Meneja wa TARURA mkoa wa Pwani, Mhandisi Ibrahimu Kibasa amesema imefanyika juhudi za kuwasiliana na Makandarasi hao kwa njia ya simu na wamekuwa hawapokei simu zake.
Amesema kuwa Kampuni ya HariCom mradi wao wa ujenzi wa barabara ya Kaunda- Kikopo yenye urefu wa Km. 0.5 ulitakiwa kuanza toka Aprili 10 mwaka jana, lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea.
Amesema Trinity toka Agosti mwaka jana mpaka sasa pamoja na kuchukuwa pesa za ‘advance’ yeye naye hajatengeneza barabara.
Katika ziara hiyo iliyoanza leo, baadhi ya maeneo miradi yake inaendelea kutekelezwa na wasimamizi wameahidi watahakikisha wanaimaliza kwa wakati.
Pia aliwataka wakazi wa Rufiji kuhakikisha wanatunza mitaro ya maji yote iliyojengwa kwa ajili ya kupitisha maji, itumike kwa matumizi hayo na sio kutupa taka katika mitaro hiyo.
Pia aliitaka halmashauri ya Rufiji kuelimisha watu juu ya usafi wa mazingira.