Featured Kitaifa

WAANDISHI WA HABARI TABORA WAPEWA MAFUNZO KUKABILIANA NA TAARIFA NA HABARI POTOFU KIPINDI CHA UCHAGUZI

Written by Alex Sonna

 

Picha ya pamoja ya washiriki wa mafunzo ya kupambana na habari potofu (fake news), misinformation na disinformation kwa waandishi wa habari mkoa wa Tabora
Mwezeshaji wa mafunzo ya kupambana na habari potofu (fake news), Kadama Malunde akitoa mada kuhusu mbinu za kubaini taarifa/habari potofu/uzushi kwa waandishi wa habari mkoa wa Tabora

 

 

Mwezeshaji wa mafunzo ya kupambana na taarifa potofu (fake news), Kadama Malunde, akiwasilisha mada kuhusu mbinu za kubaini na kukabiliana na taarifa/uzushi kwa waandishi wa habari mkoa wa Tabora.
 *
 
Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), umetoa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari mkoani Tabora yenye lengo la kupambana na changamoto za habari na taarifa potofu (fake news) hasa katika kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
 
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo ya siku mbili Oktoba 1 – 2,2025) yanayofanyika Mkoani Tabora Afisa Programu wa UTPC, Andrew Marawiti, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Ukweli Kwanza wenye lengo kuu la kuimarisha weledi wa waandishi wa habari na uimara wa wananchi dhidi ya upotoshaji wa habari hasa hasa kipindi hiki cha uchaguzi.
 
“Tunataka kuwajengea uwezo angalau waandishi wa habari 100 juu ya mbinu za kukabiliana na habari habari potofu (misinformation), upotoshaji (disinformation) uhakiki wa taarifa na mbinu za kisasa za kutumia Akili unde (Artificial Intelligence) katika kuthibitisha ukweli wa habari. 
 
Pia tunalenga kuwawezesha waandishi chipukizi, hususani wanawake, ili wawe mstari wa mbele katika mapambano haya,” amesema Marawiti.
 
Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Kadama Malunde, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Malunde 1 Blog, ametoa mada kuhusu namna ya kutambua na kupambana na taarifa na habari potofu ‘Fake News’.
 
Katika wasilisho lake, Malunde ameeleza kuwa mitandao ya kijamii imekuwa chanzo kikubwa cha kusambaa kwa taarifa zisizo sahihi, hususani katika nyakati nyeti kama uchaguzi, majanga au masuala ya afya.
 
Ametaja aina za taarifa potofu kuwa ni pamoja: Misinformation – taarifa zisizo sahihi lakini hazikusudiwi kudanganya (mfano: kusambaza picha ya tukio la zamani ukidhani ni la sasa), Disinformation – taarifa za uongo zinazotengenezwa kwa makusudi ili kupotosha (mfano: propaganda za kisiasa), Malinformation – taarifa sahihi zinazotolewa kwa nia ovu au nje ya muktadha (mfano: kutumia taarifa ya kweli kumdhalilisha mtu) na Fake News – habari za kughushi ambazo huwasilishwa kama taarifa halali (mfano: uongo kuhusu viongozi wa kitaifa).
 
Malunde amesisitiza kwamba jukumu la waandishi wa habari ni kuhakikisha hawasambazi taarifa bila uhakiki, bali wawe mabalozi wa ukweli na weledi katika jamii.
 
“Watu wengi hushindwa kutofautisha ukweli na uongo. Hali hii inachangia kusambaa kwa habari potofu ambazo huiga muundo wa habari halali kutoka magazeti au vituo vya habari, lakini hubeba maudhui ya uongo au yaliyopotoshwa. Fake News ni aina ya misinformation au disinformation ambayo huwasilishwa kama ‘habari ya kweli’, lakini kimsingi ni ya uongo, imeundwa kupotosha, kuchochea hisia au kuendeleza ajenda fulani,” ameeleza Malunde.
 
Amezitaja mbinu muhimu za kukabiliana na changamoto hiyo kuwa ni pamoja na kuepuka kusambaza taarifa mara tu unapoiona mtandaoni.
 
“Usikubali taarifa kwa urahisi; fikiria kabla ya kusambaza. Soma zaidi ya kichwa cha habari kwani mara nyingi hupotosha maana halisi ya taarifa. Kagua picha, video na maandishi kwa makini kabla ya kuamini au kusambaza”.
 
“Chanzo cha taarifa kina maana kubwa. Kabla hujaamini, hakikisha kwanza uhalali wa yule anayekuletea taarifa hiyo. Usisambaze taarifa kabla ya kuthibitisha ukweli wake ili kuepuka kusambaza upotoshaji. Tafuta taarifa hiyo kutoka kwa vyombo vya habari vinavyoaminika au wataalamu wa uhakiki wa ukweli (fact-checkers)”,ameongeza Malunde.
 
 Washiriki wamefundishwa mbinu mbalimbali za uthibitishaji wa habari, ikiwemo kutumia reverse image search kupitia Google na njia nyingine kugundua asili ya picha na video, kulinganisha taarifa na vyanzo vinavyoaminika, pamoja na kusoma zaidi ya vichwa vya habari ili kuhoji uhalisia wake.
 
Mafunzo haya yanafanyika ikiwa Tanzania inajiandaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, wakati changamoto ya upotoshaji wa taarifa mitandaoni imekuwa kubwa duniani kote.
 
UTPC inatarajia kuwa kupitia mafunzo haya yanayotekelezwa kwa kushirikiana Taasisi ya Jamii Africa, kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uholanzi – Tanzania, waandishi wa habari wataimarika katika kulinda maadili ya taaluma na kusaidia wananchi kupata taarifa sahihi, hatua itakayoongeza imani kwa vyombo vya habari na kuimarisha mchakato wa uchaguzi.

About the author

Alex Sonna