Featured Makala

MSONGO WA MAWAZO UNAVYOCHANGIA KASI YA MAGONJWA YA MOYO

Written by mzalendo

Na Gideon Gregory, Dodoma

Leo ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani kote, wataalamu wa afya nchini wameonya kuwa changamoto za afya ya akili ikiwemo msongo wa mawazo, unyogovu na hofu za mara kwa mara zinachangia kwa kiwango kikubwa kuzorota kwa afya ya moyo.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2019 zinaonyesha kuwa, takribani watu milioni 17.9 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na magonjwa ya moyo ikiwa ni sawa na asilimia 32 ya vifo vyote.

Akizungumza na Jambo FM leo Septemba 29,2025 Daktari Bingwa wa Moyo kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dkt. John Meda, anafafanua namna msongo wa mawazo unavyosababisha matatizo ya moyo.

“Kuna ugonjwa ambao moyo wako unaweza ukawa mkubwa na ukashindwa kufanya kazi kwasababu tu kumekuwa na afya ya akili, kwa maana msongo wa mawazo uliopindukia na hii utokea zaidi kwa wanawake wenye umri kati ya miaka 30 na 40 ambao moyo mara nyingi unakuwa unaenda mbio kila wakati kwahiyo moyo unatanuka unakuwa mkubwa kwasababu ya hofu na vitu vingine, “anafafanua.

Ripoti iliyotolewa na WHO Oktoba 19,2022 ilibainisha kuwa katika kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2020 mpaka mwaka 2030 inakadiriwa watu milioni 500 watakuwa wameugua magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo ugonjwa wa moyo ambapo kundi la vijana liko hatarini.

“Hili kundi la kati hapo kuanzia miaka 25 mpaka 45 tunaona wakiwa na changamoto nyingi sana za magonjwa ya moyo kwa maana ya shinikizo la juu la damu, kwahiyo unavyokuwa na shinikizo la juu la damu una umri mdogo maana yake utaishi nalo kwa muda mrefu, kwahiyo uwezekano wa moyo wako kuwa mkubwa au figo kufeli au kuingia kwenye shida ya kiharusi na vitu kama hivyo, ni niubwa,”anasema Dkt. Meda.

Kutokana na changamoto hiyo, vijana wanasema mara nyingi hutumia njia mbalimbali ikiwemo kusikiliza muziki, kucheza mpira, kuomba ushauri kwa watu wao wa karibu kama njia ya kukabiliana na msongo wa mawazo katika maisha yao ya kila siku.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa Afya, Mshauri na Mlezi wa Jamii, Dkt. Sospeter Bulugu, anatoa nasaha kwa jamii kujilinda dhidi ya changamoto hiyo ya kiafya.

“Hapa kitu ambacho mtu anapaswa kukijua ni mazingira yapi yeye anaweza au yanaweza yakamuweka kwenye hali ya usalama zaidi, kwa mfano kuangalia marafiki ambao wanaweza kutatua matatizo yanayompelekea kuwa na msongo wa mawazo, “anasema.

Anasema sababu moja wapo inayopelekea changamoto ya afya ya akili ni pamoja na kusababisha magonjwa ambayo yanayoshabihiana na eneo la moyo pamoja na kuathiri suala la mzunguko wa damu mwilini.

“Kwahiyo tunapokuja kuangalia kwamba changamoto ya afya ya akili inaweza ikapelekea vipi mtu kupata shida ya moyo maana yake tunakuwa tunaangazia kwamba huu moyo unapokuwa umeathiriwa katika namna ya uzungushaji wake wa damu ukapeleka sehemu mbalimbali za mwili basi huyu mtu anakuwa ameingia kwenye hatari ya kupatwa na changamoto ya afya ya akili,”anasema.

Dkt. Bulugu anaongeza kuwa changamoto ya afya ya akili wanapoiangalia, inaangaliwa kwa mfano mtu anayetumia dawa za kulevya anakuwa anasababisha mapigo ya moyo kwenda mbio kinyume na utaratibu, hali ambayo inaweza kupelekea moyo kushindwa kuhimili utaratibu ule ambao umesababishwa na dawa hizo.

Septemba 22, 2016 Shirika la afya ulimwenguni WHO, lilizindua mkakati wa kukabiliana na magonjwa ya moyo yakiwemo shambulio la moyo na kiharusi, magonjwa yanayoongoza kwa kusababisha vifo duniani.

Mpango huo ukiwa ni sehemu ya jitihada mpya ya kuongeza kinga na udhibiti wa magonjwa ya moyo hususani katika nchi zinazoendelea, huku umoja wa mataifa ukibainisha kuwa nchi zenye kipato kidogo huathirika zaidi na magonjwa ya moyo.

Ili kulinda afya ya moyo, wataalamu wanashauri kufanya mazoezi angalau dakika 30 kila siku, kutumia mbinu za kisaikolojia kudhibiti msongo wa mawazo, kuepuka uvutaji wa sigara, kupunguza ulaji wa chumvi na mafuta mengi, pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa afya.

MWISHO

About the author

mzalendo