Featured Kitaifa

UCHUMI WA TANZANIA UMEKUA KWA 5.4 ROBO MWAKA YA KWANZA 2025

Written by Alex Sonna

 

Na. Joseph Mahumi, WF, Dodoma

Timu ya Wataalamu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ikiongozwa na Bw. Nicolas Blancher, imemaliza ziara yake nchini Tanzania iliyofanyika kuanzia Septemba 17–24, 2025, ambapo ilifanya tathmini ya mwenendo wa Hali ya uchumi, matarajio ya kiuchumi na utekelezaji wa programu za mageuzi.

Akizungumza Bw. Blancher, katika taarifa iliyochapishwa katika tovuti rasmi ya Shirika hilo, alisema kuwa baada ya ziara yao, wameona uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa thabiti, ambapo umekua kwa asilimia 5.4 katika robo ya kwanza ya mwaka 2025 (kuanzia Julai hadi Septemba), huku mfumuko wa bei ukibaki katika kiwango cha chini cha asilimia 3.4 mwezi Agosti. Sekta za madini, kilimo, viwanda na ujenzi ndizo zimekuwa nguzo kuu za ukuaji huo.

IMF ilibainisha kuwa matarajio Chanya ikiwemo mageuzi ya mapato kupitia Mkakati wa Muda wa Kati wa Mapato (Medium-Term Revenue Strategy) yanatarajiwa kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuwezesha uwekezaji zaidi katika sekta za kijamii.

“Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kudhibiti mfumuko wa bei ndani ya kiwango cha lengo la asilimia 3 hadi 5, na hatua ya kupunguza riba kuu ya benki hadi 5.75% imesaidia kuchochea shughuli za kiuchumi“ alisema Bw. Blancher.

Aidha, aliongeza kuwa uboreshaji wa soko la fedha za kigeni umeongeza ukwasi na kupunguza tofauti kati ya soko rasmi na lisilo rasmi.

Nakisi ya akaunti ya sasa imeshuka hadi asilimia 2.5 ya Pato la Taifa katika mwaka wa fedha 2024/25, ikichangiwa na mauzo ya madini, bidhaa za kilimo na utalii. Akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani bilioni 6.2 kufikia Julai 2025, sawa na miezi minne ya uagizaji bidhaa.

IMF imesisitiza umuhimu wa kuharakisha utekelezaji wa mageuzi ili kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, ikiwa ni pamoja na kuwekeza kwenye elimu, afya, ajira kwa vijana na mageuzi ya tabianchi kupitia msaada wa washirika wa maendeleo.

IMF inatoa shukrani kwa Serikali ya Tanzania, washirika wa maendeleo, sekta binafsi na asasi za kiraia kwa ukarimu na majadiliano yenye mafanikio wakati wa ziara hiyo.

About the author

Alex Sonna