Featured Kitaifa

FCC YAIMARISHA USHIRIKIANO NA TUME YA USHINDANI YA AFRIKA KUSINI

Written by Alex Sonna

 

Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) imeingia makubaliano rasmi ya ushirikiano na Tume ya Ushindani ya Afrika Kusini (CCSA) kwa lengo la kuimarisha ulinzi wa ushindani wa haki na maslahi ya watumiaji katika nchi zote mbili.

Makubaliano hayo yalitiwa saini mwezi Septemba mwaka huu, wakati wa ziara ya kikazi ya siku tano ya viongozi wa FCC nchini Afrika Kusini. Hati hiyo ya makubaliano inalenga kushirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwemo kubadilishana taarifa, kujengeana uwezo kitaasisi, kufanya tafiti za pamoja na kuratibu utekelezaji wa sheria zinazohusu ushindani na ulinzi wa watumiaji.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa, alisema makubaliano hayo yatasaidia kuongeza nguvu ya taasisi katika kulinda maslahi ya wananchi na pia kuendeleza masoko shindani barani Afrika.

Alisema ushirikiano huo utaleta mazingira bora ya biashara kwa kuchochea ubunifu, kuongeza ufanisi na kuhakikisha haki kwa wafanyabiashara na watumiaji.

“Tunatambua na kuthamini mafanikio ya Tume ya Ushindani ya Afrika Kusini. Uzoefu wao katika kushughulikia masuala magumu ya ushindani na ulinzi wa watumiaji utakuwa nyenzo muhimu kwetu tunapoboresha mifumo ya utekelezaji hapa nyumbani,” alisema Bi. Ngasongwa.

Aidha, alisisitiza kuwa MoU hiyo si makubaliano ya kiofisi pekee, bali ni daraja la kuunganisha taasisi hizo mbili, uchumi na zaidi ya yote wananchi wake katika kufanikisha lengo la pamoja la kuwa na masoko ya haki na jumuishi.

Kwa upande wake, Kamishna wa CCSA, Bi. Doris Tshepe, aliahidi mshikamano wa karibu katika utekelezaji wa makubaliano hayo. Alisema kubadilishana utaalamu na kufanya kazi kwa pamoja kutasaidia sana kushughulikia changamoto mpya zinazojitokeza katika sekta ya ushindani na ulinzi wa watumiaji barani Afrika.

“Makubaliano haya ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda. Unaonesha dhamira ya dhati ya nchi zetu mbili kuboresha mifumo ya kisheria na kuhakikisha masoko yenye uwazi na usawa, ambayo yatalinda maslahi ya watumiaji na wafanyabiashara kwa pamoja,” alisema Bi. Tshepe.

Viongozi kutoka taasisi zote mbili walieleza matumaini yao kuwa ushirikiano huu utazaa matunda ya kweli kwa Tanzania, Afrika Kusini na ukanda mzima wa Afrika kwa kuchochea uwazi, uwajibikaji na kulinda ustawi wa watumiaji.

     

About the author

Alex Sonna