Na Gideon Gregory, Dodoma
Timu ya Dodoma Jiji imezindua wiki ya hamasa kwa mashabiki wa timu hiyo kuelekea mchezo wa mzunguko wa Tatu wa ligi kuu soka Tanzania bara dhidi ya Coastal Union utakao pigwa katika uwanja wa Jamhuri siku ya Jumamosi majira ya saa Moja usiku.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Septemba 25,2025 Afisa habari wa timu hiyo Moses Mpunga amesema hatua hiyo inalenga kuhamasisha wakazi wa Dodoma kujitokeza kwa wingi kwenda kuiunga mkono timu yao huku ikipewa jina la KANZU DAY.
“Mashabiki wote ambao watakuja kwenye mechi yetu siku ya Jumamosi, wahakikishe wamevaa vazi la Kanzu ya rangi yoyote ile ila isiwe tu nyekundu au njano maana sidhani kama nimewahi kukutana na kanzu nyekundu au njano, usjie na kanzu ya rangi hiyo lakini ya rangi yoyote wewe vaa tu hiyo siku,”amesema.
Amesema hilo ndilo vazi mama kwa mashabiki wa timu hiyo katika mchezo huo huku kwa upande wa wakina mama akisema wao wanayo mavazi yao kama hijabu, nikabu, habaya, dera na vijora na kuongeza kuwa lengo la kuchagua vazi hilo kwanza ni mchezo wao wa kwanza kwenye ligi ya msimu huu wa 2025/26 kucheza katika uwanja wa Jamhuri.
Pia Mpunga amesema wiki hiyo ya hamasa itakwenda sambamba na mbio nyepesi maalum ziliizopewa jina la Jambo Dodoma Jiji Jogingi.
“Jogingi hii au marathoni hii fupi itakuwa ni bure kabisa haina kiingilio chochote lakini sisi sasa kama waandaaji Dodoma Jiji Football Club pamoja na Jambo Group tutakupatia tisheti ya bure kuweza kukimbia katika mbio hizi,”amesema.
Mpunga ameongeza kuwa mara baada ya mbio hizo kutamatika kutakuwa na mtanange mkali utakao wakutanisha Wanywa Bia dhidi ya Wanywa Soda ikiwa ni hatua ya kwenda kumaliza utata uliopo baina ya wao hao.
Kuhusu maandalizi ya timu yao kuelekea mtanange huo amesema maandalizi yamekamilika na wachezaji wako tayari kwenda kukabiliana nao.
Mchezo huo namba 18 kati Dodoma Jiji dhidi ya Coastal Union ni wa Wanne kukutana ambapo katika mchezo wao wa mwisho katika uwanja wa Jamhuri walitoka tasa huku Dodoma Jiji wakiwa na kumbukumbu ya kutokupata ushindi mbele ya miamba hiyo kutoka Jijini Tanga.
Timu zote zimecheza michezo miwili katika msimu huu wa mashindano ya ligi kuu soka Tanzania bara ambapo Walima Zabibu wanashika nafasi ya Kumi na alama Moja kibindoni huku Wanamangushi wakiwa nafasi Sita na alama Tatu.
Mwisho.