Na. Sgt. Geofrey Jacka – DODOMA
Mkuu wa Jeshi la Magereza Nchini CGP. Jeremiah Yoram Katungu, amewataka Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza, kujiwekea malengo na kufanya tathmini ya utendaji wao, ili kujua kipi kimefanyika kwa mafanikio na ambacho hakijafanyika ili kukiwekea mikakati ya utekelezaji.
CGP. Katungu amesema hayo Septemba 25, 2025 wakati akizungumza na Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza Makao Makuu, ambapo pia aliwapongeza Watumishi wote nchi nzima kwa kazi nzuri wanazofanya, na kuhimiza wawe na uthubutu, ubunifu na kutenda haki katika utendaji wao kwani hakuna jambo lisilo wezekana.
“Kwanza kabisa niwapongeze Watumishi wote wa Jeshi la Magereza nchi nzima kwa kazi nzuri zinazo endelea kufanyika, lakini niwatake muwe na tabia ya kujifanyia tathmini wenyewe ili kujua kama malengo mliyojiwekea yanatimia, na muwe na uthubutu wa kufanya mambo kwasababu hakuna kinacho shindikana, na uzuri rasilimali zipo” alisema CGP. Katungu
Aidha, CGP. Katungu ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuliwezesha Jeshi la Magereza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kwa kulipatia vyombo vya usafiri na kupunguza changamoto iliyo kuwepo, kuwezesha kuimarisha mifumo ya kiusalama kwa kufunga vifaa vya kisasa vya upekuzi (walk through scanner) katika Magereza yetu pamoja na matumizi ya TEHAMA katika utendaji wa Jeshi.
Pia CGP. Katungu amesema, Jeshi linaendelea vizuri na matumizi ya nishati safi ya kupikia magerezani, huku likitekeleza jukumu la urekebishaji wa wafungwa kwa ufanisi na kushirikiana na Taasisi mbalimbali za Elimu kama Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) na VETA na kufanikiwa kutoa vyeti kwa Wafungwa ambavyo vitawasaidia kuajiriwa na kujiajiri pindi wamalizapo vifungo vyao.
Katika hatua nyingine CGP. Katungu, amewakumbusha Maafisa na Askari kuhusu uwepo wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, unaotarajiwa kufanyika mapema mwezi Oktoba mwaka huu, na kuwasihi kutumia haki yao ya msingi kujitokeza kupiga kura na kuchagua viongozi bora.