Featured Michezo

YANGA SC YAANZA NA MILIONI 15 ZA GOLI LA MAMA LIGI YA MABINGWA AFRIKA

Written by Alex Sonna

LUANDA, ANGOLA 

MABINGWA  wa Ligi Kuu Tanzania Bara,Timu ya  Young Africans SC, imeanza vyema kampeni zao za Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuichapa Wiliete SC ya Angola mabao 3-0 katika mchezo wa awali  uliopigwa kwenye Uwanja wa Estadio 11 de Novembro, jijini Luanda.

Bao la kwanza la Yanga lilipatikana dakika ya 31 kupitia Aziz Andabwile, aliyepiga shuti kali kutoka nje ya 18 lililomshinda kipa wa Wiliete na kupelekea Wanajangwani kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili kilishuhudia Yanga wakiongeza kasi ya mashambulizi mnao Dakika ya 72, Edmund John alifunga bao la pili kwa pasi safi ya Maxi Nzengeli, kabla ya Prince Dube kufunga la tatu dakika ya 82 akiwa ndani ya boksi baada ya kuwachambua mabeki wa  Wiliete.

 Washambuliaji wa Yanga wakikosa nafasi mbalimbali huku Dube akikosa nafasi nyingi  kabla ya kufunga bao la  tatu.

Kwa Ushindi huo  Yanga unawapa  faida kubwa kuelekea mchezo wa marudiano  unaotarajiwa kuchezwa Septemba 27,2025 katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo, Yanga wamejipatia kitita cha Shilingi milioni 15/- kupitia mpango wa Goli la Mama, utaratibu ulioanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya kuhamasisha ushindi wa timu za taifa na vilabu vinavyoshiriki michuano ya kimataifa.

Dkt. Samia amekuwa kinara wa kusapoti michezo nchini kupitia motisha mbalimbali ambazo zimezidi kuinua ari ya wachezaji na vilabu kushindana kwa ufanisi zaidi kimataifa.

Kesho Timu ya Simba SC itashuka ugenini kucheza  dhidi ya Gaborone United nchini Botswana Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika huku Azam FC itakuwa ugenini  jijini Juba nchini Sudan Kusini, kukipiga na El Merriekh Bentui na Mabingwa wa Kombe la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) Singida BS watakuwa nchini Rwanda katika dimba la Pele kuwakabil Rayon Sports. 

About the author

Alex Sonna