Na Gideon Gregory, Dodoma
Jumla ya Shilingi Bilioni 17 zimetengwa na Serikali kwaajili ya kutekeleza Mradi wa Maji wa Miji 28, ambapo Wilaya ya Chamwino ni miongoni mwa maeneo yanayonufaika ukiwa unalenga kuondoa upungufu wa maji unaofikia lita milioni 2.7 kila siku ikiwa ni hatua ya kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Wilaya hiyo.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 10, 2025, na hadi sasa umefikia asilimia 45 ambapo zaidi ya wananchi 59,000 kutoka kata 4, vijiji 7 na vitongoji 48 watafaidika moja kwa moja.
Akizungumza leo Septemba 15,2025 mara baada ya kukagua mradi huo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesisitiza suala la ubora katika utekelezaji wake ili wananchi waweze kunufaika.
“Serikali inategemea ikitoa huduma ya maji wakati huu itakaa labda miaka 20 au 30 huko ikiwa na uhakika kuwa wananchi wa Chamwino tayari wamejitoshereza kwenye maji, kama ubora uliotakiwa ndiyo utakaojengwa,”amesema.
Hivyo, RC Senyamule amesisitiza Mkandarasi pamoja na mshauri wote wasimamie kwa umakini suala la ubora wa mradi lakini kwa muda uliosalia wa miezi mitatu lazima wasimamiwe kwa ukaribu zaidi watu hao ili wajipange kwa kuongeza muda wa kufanya kazi na kuongeza mafundi ili uishe kwa wakati.
Aidha, amewaomba vijana waliopata fursa ya kunufaika na mradi huo ulioanza kutekeleza mwaka 2023 kuwa walinzi wa vifaa na kuhakikisha wanakuwa sehemu ya kusimamia ubora wa mradi huo.
Kwa mujibu wa Meneja wa DUWASA Wilaya ya Chamwino Gray Mbalikila ameeleza kuwa kwa sasa mahitaji ya maji katika Mji huo ni wastani wa lita milioni 7.5 kwa siku, huku uzalishaji ukiwa lita milioni 4.8, hivyo kusababisha upungufu mkubwa kwa wananchi.
Kukamilika kwa mradi huo kutasaidia upatikanaji wa maji safi kuongezeka kutoka asilimia 91 hadi kufikia 100, huku uzalishaji ukipanda hadi lita milioni 12.32 kwa saa 22 za uzalishaji, jambo litakalosaidia kupanua huduma hadi maeneo ya pembezoni, huku nao baadhi ya wananchi wakiiomba Serikali kusimamia vyema ili uweze kukamilika kwa wakati.
Mwisho.