Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Wana-Lindi wanakila sababu ya kumchagua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 Mwaka huu.
Amesema kuwa Rais Dkt. Samia amegusa matamanio ya Wana-Lindi kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo kwa kiasi kikubwa imegusa maisha ya kila siku ya wakazi wa mkoa huo.
Amesema hayo leo Jumamosi (Septemba 13, 2025) katika uzinduzi wa kampeni za Chama cha Mapinduzi mkoa wa Lindi na Wilaya ya Ruangwa zilizofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Likangala, Ruangwa mkoani Lindi.
“Tunayo sababu ya kuwachagua wagombea wa Chama cha Mapinduzi, sote tunafahamu namna Rais Dkt. Samia alivyotekeleza miradi katika mkoa huu, kwenye sekta za elimu, afya, maji, barabara, uwezeshaji wananchi kiuchumi. Mkoa huu tunamiradi mikubwa itakayoufanya uchangamke na kuchachua uchumi wetu”
Ameongeza kuwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Dkt. Samia ipo miradi ambayo ameitekeleza kwa ufanisi mkubwa hivyo kumpa nafasi nyingine kutamuwezesha kumalizia miradi yote iliyobaki na kuanzisha mingine ili ilete maendeleo zaidi katika mkoa huo. “Hii ni sababu tosha ya Wana-lindi kumchagua Rais Dkt. Samia”
“Katika kipindi kilichoisha Rais Dkt. Samia ameleta miradi mikubwa, ya kati na midogo, anafanya hivi kwa kutambua wananchi wanapaswa kuhudumiwa, hata ilani hii imeonesha maeneo mengine yatakayotekelezwa katika mkoa huu wa Lindi”
Amesema kuwa Wana-Lindi wanapaswa kumchagua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aendelee kutekeleza miradi ya gesi, bandari ya uvuvi Kilwa, ujenzi upya wa barabara ya Kibiti-Lindi, ujenzi wa reli ya kanda ya kusini pamoja na kuunganisha mkoa wa Lindi kwenye gridi ya Taifa umeme.
Akimnadi mgombea ubunge wa jimbo la Ruangwa Kasper Mmuya, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa mgombea huyo ni mbobevu, mtenda kazi na anahakika ataweza kufanya kazi ya kuendelea kuleta maendeleo katika jimbo hilo.
Kwa Upande wake, Mgombea ubunge wa jimbo la Ruangwa Kasper Mmuya amesema kuwa katika kipindi cha uongozi wake ataendeleza mazuri yote yaliyoanzishwa na Mheshimiwa Majaliwa ikiwemo kwenye sekta ya elimu, afya na uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Amewahakikishia wana Ruangwa kuwa atakuwa mtumishi wao na atashirikiana nao katika kila eneo ambalo litawezesha jimbo hilo kuendelea kupiga hatua kubwa za kimaendeleo.
Wagombea ubunge waliohudhuria uzinduzi huo ni pamoja na Salma Kikwete (Mchinga), Nape Nnauye (Mtama), Kinjekitile Ngombale (Kilwa Kaskazini), Asnen Dewji (Kilwa Kusini) Mohamed Utali (Lindi Mjini), Fadhili Liwaka (Nachingwea) na Msham Munde (Liwale).