Na Mwandishi Wetu
KLABU ya Yanga SC imepanga kutumia zaidi ya Shilingi Bilioni 33.6 kwa ajili ya maandalizi na ushiriki wake kwenye mashindano ya msimu ujao wa 2025/2026.
Bajeti hiyo mpya ni ongezeko la asilimia 32 ikilinganishwa na ile ya msimu uliopita wa 2024/2025, ambapo klabu hiyo iliidhinisha matumizi ya Sh Bilioni 25.6 na kutumia Sh Bilioni 25.3, huku kiasi cha zaidi ya Sh Milioni 300 kikibaki.
Akizungumza wakati wa mkutano mkuu wa klabu hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam, uongozi wa Yanga umeeleza kuwa kati ya Sh Bilioni 33.6 zilizopangwa, takribani Sh Bilioni 12 zinahitajika ili kufanikisha utekelezaji wa malengo yaliyoainishwa kwenye bajeti hiyo.
Imeelezwa kuwa fedha hizo zitatumika katika maeneo mbalimbali ikiwemo maandalizi ya timu, usajili wa wachezaji, mishahara, gharama za usafiri, posho pamoja na uendeshaji wa klabu kwa ujumla.
Uongozi wa Yanga umeeleza dhamira yake ya kuhakikisha bajeti hiyo inatekelezwa kwa ufanisi, ili timu iweze kufanya vizuri katika Ligi Kuu ya NBC, Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) na mashindano ya kimataifa ya CAF.